MAELEZO YA WAZIRI WA KILIMO KUHUSU AZIMIO LA BUNGE LA KURIDHIA ITIFAKI YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YA VIWANGO VYA AFYA YA MIMEA, WANYAMA NA USALAMA WA CHAKULA (EAC SPS)

MAELEZO YA WAZIRI WA KILIMO KUHUSU AZIMIO LA BUNGE LA KURIDHIA ITIFAKI YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YA VIWANGO VYA AFYA YA MIMEA, WANYAMA NA USALAMA WA CHAKULA (EAC SPS)

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akitoa maelezo kuhusu Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango Vya Afya ya Mimea, Wanyama na  Usalama wa Chakula (East African Community Protocol on Sanitary and Phytosanitary Measures – EAC SPS), Bungeni Jijini Dodoma Leo tarehe 8 Septemba 2021. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)


Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akitoa maelezo kuhusu Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango Vya Afya ya Mimea, Wanyama na  Usalama wa Chakula (East African Community Protocol on Sanitary and Phytosanitary Measures – EAC SPS), Bungeni Jijini Dodoma Leo tarehe 8 Septemba 2021. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

1.0       UTANGULIZI

Mheshimiwa  Spika, Ninapenda kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu lijadili na kukubali kupitisha Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango Vya Afya ya Mimea, Wanyama na  Usalama wa Chakula (East African Community Protocol on Sanitary and Phytosanitary Measures – EAC SPS)

Mheshimiwa  Spika, Chimbuko la Azimio la Kuridhia Itifaki ya EAC- SPS ni Ibara ya 151  ya Mkataba wa EAC inayoeleza kuwa nchi wanachama zitaandaa Itifaki (Protocols) katika maeneo yote ya ushirikiano pale inapobidi. Vilevile, Ibara za 105 hadi 110 za Mkataba huo zinataka nchi wanachama kushirikiana katika Sekta ya Kilimo na Chakula ambapo kwa upande wa Viwango vya SPS inataka nchi hizo kudhibiti magonjwa ya mimea na wanyama; kuwianisha Sera, Sheria na Kanuni za kudhibiti visumbufu na magonjwa; kuwianisha na kuimarisha taasisi za usimamizi na kuwianisha na kuimarisha huduma za ukaguzi na utoaji wa vyeti kwa ajili ya usafi mimea (Phytosanitary) na wanyama au bidhaa za wanyama (zoo-sanitary). Aidha, Itifaki ya Umoja wa Forodha (Customs Union) inataka ushirikiano katika eneo hili ili kukuza biashara ndani na nje ya EAC.

Mheshimiwa Spika, nchi wanachama wa EAC ziliandaa Itifaki ya SPS ikiwa ni utekelezaji wa Ibara ya 151 ili kuwianisha viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula.

Aidha, Itifaki hiyo ilisainiwa na Baraza la Sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula tarehe 12 Julai 2013 Jijini, Arusha na baadaye kuidhinishwa na Wakuu wa nchi wanachama katika Mkutano Mkuu wa 14.

2.0       WARAKA WA MAPENDEKEZO YA KURIDHIA ITIFAKI

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo iliandaa Waraka wa Mapendekezo ya kuridhia Itifaki ya EAC SPS  kwa kuhusishaOfisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Wizara mbalimbali zikiwemo Fedha na Mipango, Sheria na Katiba, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Mifugo na Uvuvi, Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii. Wadau wengine ni Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki (TPRI),

Taasisi Kilele ya Mazao ya Bustani (TAHA), Ofisi ya Hifadhi ya Mimea Zanzibar, Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Tume ya Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa  Spika, Waraka Na. 34/2013-14 wa Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya EAC SPS uliwasilishwa kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 03 Juni, 2015 ambapo Baraza liliagiza  kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iandae Azimio la Bunge kwa ajili ya Kuiridhia Itifaki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa  Chakula ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (The East African Cummunity Protocol on Sanitary and Phytosanitary Measures) na kuliwasilisha Bungeni ili liweze kuridhiwa ipasavyo.

Mheshimiwa  Spika, kabla ya hatua hii ya kuridhiwa kwa Itifaki Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi imefanya majadiliano ya kina kwa kupitia maeneo yote yanayohusu Itifaki kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja na kuainisha mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa utekelezaji wa Itifaki ili kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania.

3.0       MADHUMUNI YA ITIFAKI YA EAC -SPS

Mheshimiwa Spika, Madhumuni ya Itifaki yaliyoainishwa katika Ibara ya 2 ni yafuatayo:-

(a)                  Kukuza biashara ya chakula na bidhaa za kilimo ndani na nje ya Jumuiya;

(b)                  Kuhimiza  utekelezaji wa Misingi Mikuu ya Makubaliano ya Matumizi ya Viwango vya SPS (the WTO Agreement on the Application of Sanitary and Phytosanitary Measures) (uwianishaji (harmonisation), equivalenceregionalisationtransparency (uwazi)  na tathmini ya athari (risk assessment);

(c) Kuimarisha ushirikiano na uratibu wa viwango na shughuli za Afya ya Mimea, Wanyama na usalama wa chakula kitaifa na kikanda kwa kuzingatia uelewa wa pamoja matumizi ya viwango hivyo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; na

(d)                  Kuimarisha hadhi ya viwango vya SPS kwa kuzingatia vigezo vya kisayansi ndani ya Jumuiya.

4.0       IBARA ZA ITIFAKI NA MAUDHUI YAKE

Mheshimiwa Spika, Itifaki ina Ibara 17. Nitataja baadhi ya Ibara hizo na maudhui yake kwa ufupi ifuatavyo :-

Ibara ya 2 inahusu madhumuni ya Itifaki kama nilivyoeleza katika sehemu ya 3.0 hapo juu.

Ibara ya 3  inaeleza kuwa mawanda ya ushirikiano ni katika kutumia (adoption) viwango vya SPS kwa kuwianisha viwango vya afya ya mimea, wanyama na usalama wa chakula;

Ibara ya 4 hadi 6 zinazungumzia ushirikiano katika masuala yanayohusu afya ya mimea, wanyama na usalama wa chakula na hatua mbalimbali ambazo nchi wanachama zinapaswa kutekeleza kupitia ushirikiano huo;

Ibara ya 7 inahusu nchi wanachama kuteua  Mamlaka na/au Taasisi mahiri (competent authorities) kwa madhumuni ya Itifaki.

Ibara ya 8 inahusu udhibiti na uwezeshaji wa biashara ya chakula na bidhaa za kilimo kwenye vituo vya mipakani.

Ibara ya 9 inaeleza nchi wanachama zitashirikiana katika kubadilishana taarifa na utaalam kuhusu viwango vya afya ya mimea, wanyama na usalama wa chakula kupitia uanzishwaji na uendeshaji wa mfumo wa kikanda kuhusiana na madhumuni ya Itifaki.

Ibara ya 10 inahusu ushirikiano katika kutafuta msaada wa  kiufundi ili kujenga uwezo wa nchi wanachama katika kutekeleza viwango vya SPS;

Ibara ya 11 inahusu nchi wanachama kuwianisha Sera, Sheria, kanuni na Programu ili kufanikisha madhumuni ya itifaki;

Ibara ya 12 inahusu mfumo wa kitaasisi ambapo Baraza la Mawaziri lililoanzishwa kwa mujibu wa Ubara ya Tisa (9) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  wenye dhamana ya ushirikiano wa Afrika Mashariki litaanzisha taasisi zitakazopewa mamlaka ya kutekeleza madhumuni ya Itifaki kwa kadri itakavyoonekana inafaa;

Ibara ya 13 inahusu mamlaka ya Baraza katika kutunga Kanuni, kutoa maelekezo na kufanya maamuzi kwa kadri itakavyoonekana inafaa kwa mujibu wa madhumuni ya Itifaki hii.   

Ibara ya 14 kinafafanua kwamba Usuluhishi wa Mgogogoro (Dispute settlement) kati ya nchi wanachama kuhusu tafsiri au utekelezaji waItifaki utatatuliwa kwa mujibu wa MKATABA wa Jumuiya ya EAC;

Ibara ya 15 inatoa fursa kwa nchi wanachama kuifanyia marekebisho Itifaki hii kwa kuzingatia Ibara ya 150 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ibara ya 16 cha inaeleza kuwa Itifaki itaanza kutumika baada ya kuridhiwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya.

Ibara ya 17 inaeleza kuwa Itifaki hii na nyaraka zote za kuiridhia zitawasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye atarejesha nakala kwa nchi wanachama. Aidha, Itifaki itasajiliwa katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa zenye jukumu la kutekeleza viwango vya SPS.

5.0       AZIMIO LA BUNGE LA KURIDHIA ITIFAKI YA EAC -SPS

Mheshimiwa  Spika, Kwa mujibu wa Ibara ya 16 ya Itifaki, nchi wanachama zinatakiwa kuiridhia Itifaki hii kwa kuzingatia taratibu za nchi husika. Aidha, Ibara ya 17 inataka nchi wanachama zilizoridhia Itifaki kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya Maazimio (instruments of ratification) ya Kuridhia Itifaki hii.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepewa mamlaka ya kuridhia Itifaki hii kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

6.0       MATOKEO NA FAIDA ZA KURIDHIA ITIFAKI

Mheshimiwa  Spika, Tanzania kwa kuridhia Itifaki hii itaimarisha na kuboresha afya na usafi wa mimea, wanyama na usalama wa chakula. Utekelezaji wa Itifaki hii utaharakisha maendeleo katika Sekta ya Kilimo; ubora wa mazao, usalama wa chakula na kukua kwa biashara. Baadhi ya matokeo yatakayotokana na kuridhiwa kwa Itifaki hii ni pamoja na:

 i.            Kukua kwa biashara ya chakula na mazao ya kilimo miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya na hivyo kuongezeka kwa fursa ya bidhaa zetu kuingia kwenye soko la Jumuiya bila vikwazo ikiwa ni matokeo ya ulinganifu wa viwango vya afya ya mimea, wanyama na usalama wa chakula;

ii.            Itatoa fursa za kuimarisha ushirikiano katika kujenga uwezo wa wataalam na utafiti unaolenga viwango vya afya ya mimea, wanyama na usalama wa chakula;

iii.            Kuwezesha nchi yetu kuwa na nguvu ya pamoja na nchi nyingine katika kutetea bidhaa zinazosafirishwa kutoka ndani ya Jumuiya kuingia katika soko la kimataifa;

iv.            Kuimarisha uratibu kwa kuwa na Mwongozo wa pamoja ndani ya Jumuiya kuhusu afya ya mimea, wanyama na usalama wa chakula;

v.            Kuwepo kwa fursa ya pamoja katika Kanda ya kujilinda dhidi ya magonjwa na visumbufu vya mimea na wanyama;

vi.            Kuboresha afya na usafi wa mimea, wanyama na usalama wa chakula na hivyo kuimarika kwa maisha ya wananchi katika nchi wanachama;

vii.            Kuongezeka kwa hamasa miongoni mwa wakulima, wafugaji, taasisi na wafanyabiashara wa chakula na mazao ya kilimo katika kuongeza viwango vya ubora wa bidhaa na huduma kwa kuzingatia misingi ya kitaalamu na kisayansi ili kukidhi viwango vya afya ya mimea, wanyama na usalama wa Chakula;

viii.            Kupungua kwa vikwazo visivyo vya kiforodha mipakani vinavyohusu biashara ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kutokana na Uwazi na tathmini ya athari kulingana na makubaliano yanayohusu masuala ya viwango vya afya ya mimea, manyama na chakula;

ix.            Kuoanisha taratibu za uthibiti na ukaguzi wa mazao mipakani zitakazoondoa matakwa yasiyo ya lazima yanayoambatana na milolongo mirefu ya taratibu; na

x.            Kuimarisha utengamano wa kikanda (regionalization integration);

7.0       MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UTEKELEZAJI WA ITIFAKI

Mheshimiwa Spika, wakati wa utekelezaji wa Itifaki hii Serikali itahakikisha kuwa

i.      Uwianishaji wa Sera, Sheria na Kanuni kwa mujibu wa Itifaki hii unazingatia maslahi ya nchi na Jumuiya kwa ujumla ambapo tahadhari dhidi ya uingizaji wa mazao na bidhaa zilizobadilishwa vinasaba

(GMOs) zitaendelea kuchukuliwa kwa kuzingatia Sheria za Tanzania. Aidha, Tanzania itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki haitumiki kama eneo la kuingiza bidhaa na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zinazoweza kuhatarisha usalama wa chakula, usalama wa nchi, wanyama na mazingira.

ii.    Baada ya kuridhiwa kwa Itifaki, Serikali itaendelea kuzijengea uwezo taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa Itifaki hii hususan uwezo wa wataalam, utafiti, miundombinu, vifaa na vitendea kazi.

iii.  Mpango wa kutoa elimu utawekwa kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama vile radio, luninga, vipeperushi na magazeti.

Pia elimu itatolewa kupitia mitandao ya kijamii, uchapishaji wa majalada na tovuti za Serikali.

8.0    Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kuwasilisha Azimio hili kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ifuatavyo:-

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Translate »