Waziri Mkenda ametembelea na kufanyamazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI nchini Burundi.

Waziri Mkenda ametembelea na kufanyamazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI nchini Burundi.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda tarehe 19 Octoba 2021 ametembelea na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI ambacho kupitia kampuni yake ya ITRACOM imeanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea Jijini Dodoma nchini Tanzania. Katika ziara hiyo Waziri Mkenda pamoja na wataalamu mbalimbali aliombatana nao amekagua kiwanda cha FOMI na

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akiwa ameambatana na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide akipokelewa na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI kilichopo chini ya kampuni ya ITRACOM mjini Bujumbura, tarehe 19 Octoba 2021 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Burundi.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akiwa ameambatana na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide akikagua mbolea mbadala ya kukuzia aina ya Fomi Imbura wakati alipotembelea na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI kilichopo chini ya kampuni ya ITRACOM mjini Bujumbura, tarehe 19 Octoba 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda tarehe 19 Octoba 2021 ametembelea na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI ambacho kupitia kampuni yake ya ITRACOM imeanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea Jijini Dodoma nchini Tanzania.


Katika ziara hiyo Waziri Mkenda pamoja na wataalamu mbalimbali aliombatana nao amekagua kiwanda cha FOMI na kuona kinavyofanya kazi ikia ni lengo la kuona uwezekano wa kiwanda hicho kama kinaweza kuuza mbolea yake Tanzania kwa bei nafuu kwa wakulima na kupatikana kwa wingi na kwa wakati.


Prof Mkenda amesema kuwa kiwanda hicho nchini Burundi kinazalisha Tani kati ya 120,000 mpaka Tani 150,000 kwa mwaka kulingana na soko la mbolea huku kikiwa kimeanza ujenzi wa kiwanda cha kisasa Jijini Dodoma nchini Tanzania ambapo kitapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Tani 600,000 za mbolea ambazo ni zaidi ya mahitaji ya mbolea nchini Tanzania ambayo ni kati ya Tani 400,000 mpaka Tani 500,000 kwa mwaka.


Amesema kuwa wakati serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea Tanzania vilevile inaendelea na mkakati wa kuhakikisha kuwa inatafuta mbolea inayoweza kupatikana kwa wakati na kuwafikia wakulima kwa bei nafuu.


Waziri Mkenda amemuhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Bw Ntirampeba Simon kuwa serikali ya Tanzania itakuwa bega kwa bega kuhakikisha kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unakamilika kwa wakati uliokusudiwa.


“Wawekezaji wote wanaowekeza kwenye biashara ya Pembejeo Tanzania tunawahakikishia kuwa Tanzania ni nchi salama kwa uwekezaji hivyo wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuwekeza” Amekaririwa Waziri Mkenda.


Kwa upande wake Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide amesema kuwa mazungumzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yameongeza wigo mpana Zaidi kwa kubadilishana mawazo katika sekta ya kilimo. 

Dkt Rurema amesisitiza kuwa katika muktadha wa kuongeza uzalishaji na tija katika mazao ya kilimo kuna mambo muhimu mawili ya kuzingatia ambayo ni maji, ardhi na mbolea na katika nchi ya Burundi sekta ya mbolea imeimarika na uzalishaji unatosheleza mahitaji ya wakulima.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha Mbolea cha FOMI kilichopo chini ya kampuni ya ITRACOM Bw Ntirampeba Simon amesema kuwa Menejimenti ya kiwanda hicho imeendelea kufurahishwa sana kwa ushirikiano unaoonyesha wa viongozi wakuu wa Tanzania kwa kutembelea Burundi mara kwa mara hususani kukitambua na kukithamini kiwanda hicho.


Amesema kuwa mbolea inayozalishwa kiwanda hapo ni nzuri na inayohimili hali yoyote ya hewa na ardhi kwa mujibu wa utafiti walioufanya.


Awali Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi ambapo amewapongeza kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya huku akiwasihi kuhakikisha kuwa wanaendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza akizungumza na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi wakati alipotembelea Ubalozini ili kujionea utendaji kazi pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wote, tarehe 19 Octoba 2021.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi akitoa taarifa ya Balozi kwa Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda kuhusu utekelezaji wa majukumu ya ubalozi nchini Burundi wakati wa ziara ya kikazi ya waziri ya siku mbili Mjini Bujumbura, tarehe 19 Octoba 2021. 
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mjini Bujumbura nchini Burundi.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi amemuhakikishia Waziri Mkenda kuwa Ubalozi unaendelea kuwa kiungo muhimu katika juhudi za serikali ya Tanzania za kuhakikisha Burundi kama nchi jirani inaendelea kuwa na Amani.


Ameongeza kuwa, ubalozi unatekeleza Diplomasia ya uchumi kwa kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo Burundi ambazo watanzania wanaweza kunufaika nazo, kutafuta masoko ya mazao ya kilimo pamoja na bidhaa za viwandani za Tanzania, kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali baina ya Tanzania na Burundi yenye maslahi kwa nchi zote mbili.

wakati huo huo Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohelo Mjini Bujumbura nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 19-20 Octoba 2021.


Katika kikao kazi hicho Waziri Mkenda na Waziri Rurema wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa mifumo ya utoaji ruzuku kwenye pembejeo za Kilimo ambapo wametilia mkazo kuhusu uwezekano wa mbolea mbadala ya kupandia inayozalishwa nchini Burundi aina ya Fomi Imbura kusafirishwa kwa ajili ya matumizi ya wakulima wa Tanzania.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda (Kulia) takisisitiza jambo mbele ya Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohelo Mjini Bujumbura nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide (Wa Pili Kushoto) mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohelo Mjini Bujumbura nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Ndg Enock Nyasebwa (Wa Pili Kulia), Kaimu Balozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi (Kulia) pamoja na mtaalamu wa udongo Dkt Catherine Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Kilimo-TARI Mlingano kilichopo mkoani Tanga (Kushoto).
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda (Kulia) tarehe 19 Octoba 2021 akikabidhiwa zawadi ya kahawa na mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohelo Mjini Bujumbura nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 19-20 Octoba 2021.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda (Wa Tatu Kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide (Wa tatu Kushoto), Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Ndg Enock Nyasebwa (Kulia), Kaimu Balozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi (Wa Pili Kulia), Mtaalamu wa udongo Dkt Catherine Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Kilimo-TARI Mlingano kilichopo mkoani Tanga (Wa Pili Kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania Dkt Stephan Ngailo (Kushoto).


Katika majadiliano hayo pia Mawaziri hao wamezungumzia swala la biashara ya Mazao huku mkazo mkubwa ukiwa katika biashara ya mahindi ambayo yanazalishwa kwa wingi nchini Tanzania na soko lake likiwa halitoshelezi.


“Kuna umuhimu wa kufungua masoko hapa Burundi kwa ajili ya kufanya biashara ya mahindi kuona namna ya kuwauzia mahindi hayo ambayo mengi yanapatikana katika mikoa jirani ya Katavi na Rukwa” Amesisitiza Waziri Mkenda.


Majadiliano hayo yamejikita pia kuhusu kufanya ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi katika maswala ya Utafiti wa mazao ya Kilimo kwani ndio msingi wa mafanikio ya wakulima katika nchi zote hizo mbili.


Akizungumzia ziara hiyo nchini Burundi waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa, ziara hiyo ni muendelezo wa kuimarisha ushirikiano na uhusiano baina ya Tanzania na Burundi ambayo ni kazi inayofanywa kwa kiasi kikubwa na wakuu wa nchi zote mbili.


“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan alitembelea Burundi hivi karibuni, Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe Dkt Philiph Mpango alifanya ziara hapa pamoja na Waziri Mkuu kassim Majaliwa hii ni kuonyesha kwamba tuna mahusiano makubwa zaidi ya kisiasa na kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili” Amekaririwa Waziri Mkenda.


Prof Mkenda amemshukuru mwenyeji wake Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide kwa kuahirisha kushiriki shughuli zinazoendeela za bunge kwa ajili ya kuambatana naye katika ziara hiyo ya kikazi.


Katika ziara hiyo Waziri wa Kilimo ameambatana na Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Bw Enock Nyasebwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania Dkt Stephan Ngailo pamoja na mtaalamu wa udongo Dkt Catherine Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Kilimo-TARI Mlingano kilichopo mkoani Tanga.


Kadhalika, kwa upande wa ubalozi, ameongozana na Kaimu Balozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi.

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Latest Posts

Top Authors

Most Commented

Featured Videos

Translate »