WIZARA HII NI YA JAMII LAZIMA KWENDA ‘SITE’- WAZIRI GWAJIMA

WIZARA HII NI YA JAMII LAZIMA KWENDA ‘SITE’- WAZIRI GWAJIMA

Na WMJJWM, Dar es Salaam Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara hiyo itaendelea kufuatilia utekelezaji wa Sera na Sheria inazozisimamia huku yeye mwenyewe akiwa mstari wa mbele kwenda saiti za jamii kusikiliza na kutatua changamoto za jamii. Mhe. Dkt. Gwajima ameyasema hayo akifungua jengo la

Na WMJJWM, Dar es Salaam


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara hiyo itaendelea kufuatilia utekelezaji wa Sera na Sheria inazozisimamia huku yeye mwenyewe akiwa mstari wa mbele kwenda saiti za jamii kusikiliza na kutatua changamoto za jamii.


Mhe. Dkt. Gwajima ameyasema hayo akifungua jengo la ofisi ya kikundi cha kijamii kinachoitwa Sauti ya Jamii katika Kata ya Kipunguni jijini Dar salaam tarehe 19 Oktoba, 2022.


Amesema vitendo vingi vya ukatili vinatokea kwenye jamii kwa asilimia kubwa ikiwa ni nyumbani hivyo Jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa nyumbani kunakuwa sehemu salama kwa watoto.
“Naambiwa kwamba taarifa zinaonesha kuna kushamiri kwa matukio ya ukatili, watu wanauana kwenye jamii, watoto na wanawake wanakatiliwa kwenye jamii, wanaume pia wanasema wanakatiliwa huku takwimu za mwaka 2021 zikionesha watoto 11499 walikatiliwa ambapo kati yao 5899 walibakwa. Asilimia 60 wamebakwa majumbani kwao na asilimia 40 mtaani na mashuleni” amesisitiza Mhe. Dkt. Gwajima.


Mhe. Dkt. Gwajima amesisitiza kwamba, hatakubali kuletewa taarifa ofisini, atakwenda kujionea mwenyewe yanayofanyika kwenye jamii na hatua za mifumo iliyowekwa iwapo inafanya kwa ufanisi kwani kuna maeneo mengine utekelezaji haupo vizuri au haupo kabisa au unasuasua hivyo ni jukumu la Wizara yake kufuatilia utekelezaji wa Sera na miongozo mbalimbali katika ngazi mbalimbali nchini.
“Hatutaki kuletewa namba tukazikariri, bila kuwa tumeenda kuona kinachoendelea kwenye mitaa mbalimbali ya jamii, kama kuna changamoto tuzisikie, tuzijadili na tuwaeleze wanachotakiwa kufanya” amesisitiza Dkt. Gwajima.


Halikadhalika amezitaka kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zilizopo ngazi za kata, mitaa na vijiji kuiga mfano wa ubunifu wa kikundi cha Sauti ya Jamii kwa kuwa na shughuli zinazowaimarisha kiuchumi hivyo kutatua changamoto ya umaskini ambao ni chanzo kimojawapo cha vitendo vya ukatili.


Amesisitiza kuelimisha wananchi kuzifikia na kuzitumia fursa mbalimbali zinazopatikana nchini ili kujikwamua kiuchumi akibainisha mifuko na programu 85 zilizoainishwa kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi chini ya uongozi wa Bi. Beng’i Issa, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hili. 


Awali akieleza kuhusu kikundi hicho mmoja wa wajumbe wa kikundi hicho Juma Rashid amesema waliamua wao wenyewe kuanzisha kikundi kwa lengo la kujiinua kiuchumi kupitia fedha zao wenyewe na hatimaye kujenga ofisi hiyo kwa gharama ya zaidi ya mil 11, yenye chumba cha mafunzo ya cherehani na ujasiriamali.


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kipunguni Mhe. Steven Mushi ameipongeza Serikali kwa juhudi za kuwawezesha wananchi hasa kwa kata ya Kupunguni ambapo jumla ya mikopo ya Halmashauri iliyotolewa kwa mwaka wa fedha 2021/22 ni zaidi ya sh.  Milioni 500.
“Kwenye Kata yetu hadi sasa tuna zaidi ya vikundi 50 na bado maombi ni mengi, tunashukuru pia kwa mfumo mpya wa kielekroniki utarahisisha kupata kwa wakati na kuondoa urasimu” amesema Mushi. 


Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng’wizalubi Ludigija amesema jitihada za Waziri Mhe. Gwajima za kuingia ndani ya jamii zimesaidia kufanya wanajamii kuifahamu Wizara na majukumu yake tofauti na hapo awali.


Amesisiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kutokomeza vitendo vya ukatili kwa maendeleo na ustawi wa jamii na vizazi vijavyo.

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Latest Posts

Top Authors

Most Commented

Featured Videos

Translate »