DK. MWINYI: WAGONJWA WOTE WATIBIWE HAPA IKISHINDIKANA WAPELEKWE DAR ES SALAAM, SIO INDIA

DK. MWINYI: WAGONJWA WOTE WATIBIWE HAPA IKISHINDIKANA WAPELEKWE DAR ES SALAAM, SIO INDIA

                                                STATE HOUSE ZANZIBAR                                       OFFICE OF THE PRESS SECRETARY                                                       PRESS RELEASE Zanzibar                                                                                                                Machi 10, 2021 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema wakati umefika kwa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kuondokana na utaratibu wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu,

                                                STATE HOUSE ZANZIBAR

                                      OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

                                                      PRESS RELEASE

Zanzibar                                                                                                                Machi 10, 2021

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema wakati umefika kwa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kuondokana na utaratibu wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu, na badala yake fedha zinazotumika zielekezwe kuimarisha vitengo vya tiba katika Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini hapa wakati alipozungumza na Viongozi na watendaji wa Wizara hiyo katika mkutano uliojadili utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu wakuu wakati alipowaapisha.

Amesema kwa muda mrefu Wizara hiyo imekuwa na utaratibu wa kupeleka nje ya nchi idadi kubwa ya wagonjwa kwa matibabu , wakiwemo wale wenye uwezekano wa kutibiwa nchini na hivyo kuilazimu Serikali kutumia fedha nyingi, ikiwemo posho la kujikimu wao na madaktari  wanaowasindikiza.

Alieleza kuwa hatua ya kupeleka wagonjwa nje ikiwemo India , inapaswa kufanyika pale pasipo budi na kubainisha kuwa wagonjwa watakaoshindikana kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja watapaswa kupelekwa Hospitali za Tanzania Bara.

Alisema fedha zinazotumika kupeleka wagonjwa hao zinapaswa kuelekezwakatika kuviimarisha vitengo vya tiba vilivyopo katika Hospitali ya Rufaa  Mnazimmoja.

Aidha, aliitaka Idara ya Kinga kutoa kipaumbele katika uimarishaji wa vitengo kwa kuvipatia vifaa, akibainisha kuwepo madaktari wenye uwezo mkubwa kiutendaji.

Aliwataka wataalamu wa Wizara hiyo kukaa chini na kuishauri serikali nini kufanyike ili kuondokana na changamoto ya kuwepo kiwango kikubwa cha vifo vya watoto wachanga, wakati ambapo takwimu zikizonyesha kuwepo wastani wa watoto wachanga 23 wanaofariki kwa kila vizazi 1,000.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alisema wakati umefika kwa serikali kutafuta njia za kuanzisha huduma za Bima ya Afya, kwa kuzingatia kuwa Bajeti ya Serikali haiwezi kukidhi mahitaji ya kila jambo.

“Hatuwezi kutoa huduma za Afya kwa ufanisi kwa kutegemea fedha za Serikali pekee”, alisema.

Alieleza kuwa pamoja na Sera ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 kubainisha upatikanaji bure wa huduma za Afya nchini , alisema hatua hiyo inapaswa kuendelezwa kwa ajili ya wananchi wasio na uwezo, sambamba na wale wenye uwezo kutumia huduma za Bima ya Afya, hivyo akawataka viongozi wa Wizara hiyo kukaa chini na kuanza kufikiria uanzishaji wa huduma hiyo.

Aidha, alisema ni jambo gumu kwa Serikali kumpatia mgonjwa kila aina ya dawa bure, hivyo akataka juhudi zaidi zifanyike ili kuwa na vyanzo zaidi vya mapato kusaidia utoaji wa huduma bora za afya. 

Akizungumzia suala la upatikanaji wa dawa, Dk. Mwinyi alisema eneo hilo lina matatizo makubwa, hivyo akiitaka Bohari Kuu ya Dawa kubeba jukumu la ununuzi na usambazaji wa dawa hizo, kazi ambayo hivi sasa inafanywa na Wizara.

Alisema kuna umuhimu wa kutizama matatizo yaliopo na kuyapatia ufumbuzi, akibainisha kuwa Hospitali ndio yenye taarifa sahihi za kuelewa matatizo waliyonayo na sio Wizara,  akatoa mfano wa tenda ya ununuzi wa vifaa (vyuma) kwa ajili ya tiba ya wagonjwa mifupa iliochukuwa miezi kutokana na utaratibu huo.

Aliitaka Bohari ya Dawa ipewe jukumu la kuagiza na kusambaza dawa zote na kusema huo ndio mfumo uliokamilika, hata hivyo alishangazwa na taarifa za kuwa Bohari hiyo haina mfumo wa kumbukumbu kupitia Komputa.

Aidha, alieleza umuhimu wa kuangalia mahitaji yaliopo wakati wa kufanya ajira ili kuondokana na tatizo la upungufu wa wafanyakazi linaloonekana kujitokeza katika baadhi ya vitengo na Idara zake.  

Aliitaka Wizara hiyo kufanya juhudi za ziada ili kupata fedha zitakazowezesha kuondokana na changamoto ya Ofisi Kuu Pemba ya kukosa huduma za uchomaji taka (incinerator) katika Hospitali za Abdalla Mzee, Wete pamoja na Vitongoji, ili kuondokana na taka hatarishi.

Akigusia changamoto zinazozikabili  Idara mbali mbali za Wizara hiyo, Dk. Mwinyi aliitaka Wizara hiyo kuwa na mifumo ya pamoja kwa kuzingatia kuwa tayari Serikali ilitoa fedha nyingi ili kufanikisha kazi hiyo ambayo haikufanyika ipasavyo.

Aliutaka Uongozi wa Wizara hiyo kuliangalia suala hilo kwa kina ili kubaini usahihi wa matumizi ya fedha hizo na jinsi zilivyotumika, wakati huu  mitandao ikiwa haifanyikazi.

Vile vile, Dk. Mwinyi akautaka Uongozi huo kufikiria uwezekano wa kuziungnisha taasisi za Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi na ile ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuwa taasisi moja kwa dhamira ya kuleta ufanisi na kuondoa urasimu.

Kuhusiana na miradi ya maendeleo ya Wizara hiyo, alitaka juhudi zifanyike kutafuta mikopo kutoka mashirika ya Kimataifa ili kupata fedha zitakazowezesha kufanikisha miradi hiyo kwa kuzingatia ukubwa wa gharama, huku akitaka fedha za Bajeti zitumike kulipia mikopo hiyo.

Aliwataka viongozi hao kutathmin uamuzi wa Serikali wa kuifanyia ugatuzi sekta ya Afya katika Manispaa za Wilaya, iwapo umeleta ufanisi, akibainisha umuhimu wa kufanya ugatuzi wenye kuleta tija, sambamba na kuwataka kuendeleea kuvutia wahisani ili kuimarisha  huduma za Afya nchini.

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dk. Omar Dadi Shajak alisema katika kufanikisha utatuzi wa  changamoto ziliopo, Wizara hiyo imeandaa mipango kadhaa kwa lengo la kuimarisha mazingira ya utendaji kazi, ikiwemo  kuweka utaratibu wa kuanzisha mifumo ya TEHAMA itakayounganisha mifumo iliopo ili kupunguza  gharama ya kuwepo mifumo mingi.

Alisema Wizara inalenga kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa, Mkoa na Wilaya, ambapo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara maalum za SMZ itavijengea uwezo vituo vya Afya vya msingi pamoja na vituo vya madaraja ya kwanza na pili ili kutoa huduma kwa saa 24.

Alisema Wizara itaifanyia ukarabati mkubwa Wodi ya Mifupa, chumba cha upasuaji pamoja na kufanya marekebisho ya miundombinu ya Hospitali, sambamba na kununua mashine na samani.

Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ina jumla ya wafanyakazi wa kada mbali mbali 5,062 Unguja na Pemba, ambapo kw amujibu w atakwimu za mwaka 2020 ian jumla ya  madaktari 345, wauguzi 1,328. 

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alifika Hospitali kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kuwakagua majeruhi wa ajali ya gari iliyotokea asubuhi ya leo huko Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja ambayo imewahusisha wafanyakazi wa kitengo cha habari cha Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Akiwa ameongozana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuwakagua majeruhi hao waliopata ajali hiyo na kuwaombea kupona kwa haraka huku akimuombea kwa Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema peponi mmoja wa wafanyakazi hao aliyefariki dunia.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Translate »