WAZIRI SIMBACHAWENE ASEMA KATI YA MAJAMBAZI KUMI WANAOKAMATWA NCHINI, WATATU WANATOKA GEREZANI, WANARUDIA TENA KUFANYA UHALIFU

WAZIRI SIMBACHAWENE ASEMA KATI YA MAJAMBAZI KUMI WANAOKAMATWA NCHINI, WATATU WANATOKA GEREZANI, WANARUDIA TENA KUFANYA UHALIFU

Na Barnabas Kisengi-Kibakwe. WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema katika operesheni ya kuwasaka majambazi inayoendelea nchini kati ya majambazi kumi wanaokamatwa mitaani, watatu wanatoka gerezani. Amesema kuwafunga majambazi hao hakusaidii sana kwasababu wanarudi mitaani na kuendelea kufanya uhalifu wa aina mbalimbali pamoja na kuwaua watu wenye haki, hivyo watatafuta namna nyingine

Na Barnabas Kisengi-Kibakwe.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema katika operesheni ya kuwasaka majambazi inayoendelea nchini kati ya majambazi kumi wanaokamatwa mitaani, watatu wanatoka gerezani.

Amesema kuwafunga majambazi hao hakusaidii sana kwasababu wanarudi mitaani na kuendelea kufanya uhalifu wa aina mbalimbali pamoja na kuwaua watu wenye haki, hivyo watatafuta namna nyingine ambayo watamalizana na majambazi hayo.

Waziri Simbachawene amezungumza hayo, leo, katika Kata ya Pwaga, Jimbo la Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, katika ziara yake inayoendelea ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni kwake, ambapo amesema licha ya kuwa wamemalizana na majambazi hayo lakini bado Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni ya kuwasaka itakayo kamilika Julai 28, mwaka huu.

“Ukikamata majambazi kumi, watatu wametoka gerezani, ama kwa msamaha au kwa kumaliza kifungo, wanarudi tena kufanya uhalifu, sasa tutaendelea kuwafunga wanarudi kufanya uhalifu, tunawafunga wanarudi kuua watu wenye haki, hapana, nasisi tutatafuta namna ambayo tutamalizana vizuri,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, “Unapopigania uhai wa watu wenye haki kwa njia yoyote ile wala hautendi dhambi, kwahiyo tutajua namna tutakayomalizana, na mimi nawaambia, Rais Samia alisema siku ile tusibonyezeke, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Rais hatujabonyezeka, walipotubonyeza tuliponyanyuka juu hatukubonyezwa tena,  tumehakikisha mpaka tumeelewana Kiswahili, kwa hiyo tumemalizana tunaenda vizuri, na narudia kusema tena waache waamue kufanya kazi halali.”

Aidha, Waziri Simbachawene amesema wanaohusika na uhalifu ni watu wanaotoka katika jamii, wananchi wanawajua, ili kudhibiti matukio ya uhalifu wananchi hao wanapaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wanaofanya uhalifu huo katika sehemu wanazoishi.

Amesema baadhi ya wahalifu hao wanavamia maduka ya mpesa, tigopesa, airtel money na mengineyo, wanachukua fedha, hatua ambayo inaleta taharuki mitaani ambapo amewataka wananchi wajue kuwa majambazi hayo wanapofanya uvamizi huo katika maduka hayo, wanapaswa kujua wamevamiwa wao hivyo wanapaswa kushirikiana ili kupinga hatua hiyo.

“Ndugu zangu ukiona jirani yako au mtu anayewapa huduma hapa kijijini amevamiwa, na nyinyi kijijini kizima mtakuwa mmevamiwa, mtu anaporwa na majambazi wanatumia silaha, lakini nyinyi mnaona kama kitu cha kawaida tu, Wamasai wale akiibiwa mfugaji mmoja ng’ombe wanatoka wote kusaka huyo aliyeiba, lakini jambazi hawezi kutoka kwingine kokote kama hana ‘connection’ na mtu wa hapa, kwahiyo wapo vijana mitaani ni madalali wa majambazi na nyie lazima mnawafahamu, kwahiyo dawa ni kutoa taarifa Polisi.”amesema simbachawene

Waziri simbachawene amesema Jeshi la Polisi haliwezi kuwa na askari kila mahali ni jukumu la wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi  kwa ajili ya usalama wao kwa kutoa taarifa sahihi juu ya uhalifu na wahalifu, lakini pia kwa kushiriki katika ulinzi pamoja na Jeshi la Polisi na ndiyo tunaita ulinzi shirikishi.

Aidha amesema  kuwa, hivi karibuni kulikuwa na majambazi yalisikika katika baadhi ya Miji hapa Nchini lakini tulishughulika nao kwa kuwa Serikali ipo imara na haijaribiwi na wamepata majibu.

Pia amewataka Watanzania kufanya kazi halali kwa kuwa fursa zipo nyingi nchini kuliko kufanya uhalifu ambao utawaletea matatizo makubwa na kamwe hawawezi kufanikiwa kwa kufanya shughuli isiyo halali.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Pwaga, Jimbo la Kibakwe, Wilfred Mgonela, alimshukuru Mbunge huyo kwa kufanya ziara katika kata yake, na pia alimuomba aweze kutatua shida ya maji ambayo imekuwa kero ndani ya Kata hiyo na madawati  katika shule ya ya secondary pwaga. 

Waziri Simbachawene amemaliza ziara yake ya siku mbili jimboni kwake ambapo aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anapenda watu wafanye kazi, na alisisitiza kuwa ili wananchi hao wafanikiwe katika Maisha yao njia pekee ni kufanya kazi kwa juhudi ikiwemo kufanya kilimo pamoja na shughuli zingine halali.

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Translate »