Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma. Changamoto kubwa ya wakulima nchini ni pamoja na kutotumia mbinu za kilimo bora kama vile kutotumia mbegu bora, kutozingatia nafasi kati ya mmea na mmea, kutotumia mbolea kwa usahihi na matumizi hafifu ya viuatilifu. Katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali imeanzisha kituo mahiri kitakachowasaidia wakulima kuongeza ufahamu wa kanuni
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma.
Changamoto kubwa ya wakulima nchini ni pamoja na kutotumia mbinu za kilimo bora kama vile kutotumia mbegu bora, kutozingatia nafasi kati ya mmea na mmea, kutotumia mbolea kwa usahihi na matumizi hafifu ya viuatilifu.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali imeanzisha kituo mahiri kitakachowasaidia wakulima kuongeza ufahamu wa kanuni za kilimo bora kwa wadau hususani wakulima na kuongeza ushirikiano kati ya wakulima, wagani, watafiti na wadau wa mbegu.
Waziri wa Kilimo, Mhe Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 24 Septemba 2021 wakati akizindua Kituo Mahiri cha Usambazaji Teknolojia za Kilimo kilichopo Nzuguni, kilicho chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Jijini Dodoma.
Amesema kuwa kituo hicho kimeanzishwa muda muafaka wakati Wizara ya Kilimo imeweka mkakati wa kuimarisha huduma za ugani nchini.
Waziri Mkenda ametoa rai kwa viongozi wa mikoa iliyo katika kanda ya kati kukitumia kituo hicho kuwajengea uwezo kwa vitendo maafisa ugani ili wasaidie kuwajengea uwezo wakulima katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza uzalishaji na tija, kuchangia kuwa na uhakika wa chakula, kipato, lishe bora na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa kituo hicho mahiri cha kusambaza teknolojia za kilimo kilichopo kwenye viwanja vya maonesho vya Nzuguni Jijini Dodoma kitatoa mafunzo ya matumizi ya teknolojia za kilimo bora kama vile matumizi ya mbegu bora, kupanda kwa nafasi pamoja na matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa “Matarajio yangu kituo hiki kitakuwa chachu ya kuwaunganisha wadau wa kilimo na masoko, pia kuanzisha kanzidata ya masoko ya mazao mbalimbali”.
“Nawasihi viongozi wa Halmashauri zote kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuendesha shughuli za uhaulishaji/usambazaji wa teknolojia bora za kilimo na kuimarisha huduma za ugani nchini” Amesisitiza Waziri Mkenda.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dodoma Mhe Riziki Lulida pamoja na kumpongeza waziri wa Kilimo lakini pia ameiomba serikali kuhimiza mikakati ya uzalishaji wa alizeti kwa wingi kwa kutoa fedha za mikopo kwa wanawake na hususani wakulima ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo.
Mhe Lulida amesema kuwa serikali imefanya kazi kubwa katika kuwanufaisha wafanyakazi wa serikali na kutambulika hivyo inapaswa kuongeza msisitizo wa kuwapatia vitendea kazi na kuwatambua maafisa ugani kutokana na kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwa manufaa ya wakulima wote nchini.
Awali, akitoa taarifa ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini- TARI Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Dkt Geofrey Mkamilo amesema kuwa njia pekee ya wakulima kuongeza kipato ni pamoja na kuzingatia taratibu zote za kilimo ikiwemo kupata mafunzo ya kilimo yanayotolewa katika vituo 17 vya utafiti wa kilimo vilivyopo nchini..
Amesema kuwa TARI imekuja na mkakati wa kuhakikisha kuwa wakulima wanaelimishwa kuhusu matumizi ya zana bora za kilimo, kupanda kwa kufuata taratibu elekezi zinazotolewa na wataalamu ikiwemo kujifunza teknolojia sahihi zitakazoleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo.
Leave a Comment
Your email address will not be published. Required fields are marked with *