Rais Dkt. Mwinyi amefungua Hoteli ya Kitalii ya Marjani Resort & SPA Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Rais Dkt. Mwinyi amefungua Hoteli ya Kitalii ya Marjani Resort & SPA Mkoa wa Kaskazini Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa pongezi kwa Wawekezaji  waliowekeza katika maeneo mbali mbali nchini, kwa kuwa na ushirikiano  wa karibu na jamii inayowazunguka katika kusaidia utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo na kijamii, hususan katika sekta za afya, elimu na huduma za maji safi na

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa pongezi kwa Wawekezaji  waliowekeza katika maeneo mbali mbali nchini, kwa kuwa na ushirikiano  wa karibu na jamii inayowazunguka katika kusaidia utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo na kijamii, hususan katika sekta za afya, elimu na huduma za maji safi na salama.

Dk. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo katika hafla ya Ufunguzi wa Mradi wa Hoteli ya Kitalii ya Nyota Tano ya Marijani Resort & SPA iliopo Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema moja ya njia ya kujenga mahusiano mema kati ya Wawekezaji na wananchi ni kujenga utamaduni wa kurejesha sehemu ya faida wanayopata kwa jamii ili kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa njia mbali mbali.

Aidha, alisema kuwepo kwa mfululizo wa matukio ya Uwekaji wa mawe ya msingi pamoja na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya Hoteli hapa nchini ni mafanikio ya juhudi za Serikali za kuvutia Wawekezaji hapa nchini, ikiwa ni kielelezo cha kuvutiwa na sera na mipango iliopo.

Alisema juhudi za pamoja kati  Serikali na wadau wa Utalii pamoja na kuwepo kwa amani na utulivu nchini, ni mambo yanayoendelea kuvutia Wawekezaji.

Alimpongeza Mwekezaji na wanahisa  wenzake kutoka Mauritius  ambao ni Kampuni za Avenes Limited, Harwood Limited na Amcop Investment Limited kwa uamuzi wao wa kuwekeza hapa nchini katika mradi mkubwa wenye hadhi unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 10.5, na akatumia fursa hiyo  kuwahakikishia mitaji na amana zao kuwa salama.

Aidha, Dk. Mwinyi aligusia suala la usalama wa watalii na kusema  ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali, hivyo akawahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuendelea kufanyakazi kwa karibu na Wawekezaji walio katika maeneo yao ili kubaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Aliitaka Mikoa hiyo kuwa na mipango thabiti ya kupambana na vitendo vyote vinavyoweza kurudisha nyuma juhudi za kukuza utalii, kuharibu utamaduni pamoja na kuipa nchi sifa mbaya.

Aliwapongeza wamiliki wa Hoteli hiyo kwa kuonyesha nia ya kununua bidhaa zote zinazopatikana hapa nchini.

Nae,Waziri wa Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga alisema mradi huo una manufaa makubwa  kwa wananchi wa maeneo hayo na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla na kupongeza juhudi na miongozo ya Rais Dk. Mwinyi kuwa imekuwa chachu  katika kuvutia Wawekezaji.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahamoud alisema katika kufanikisha dhamira ya kupunguza ajali na kuimarisha usalama wa watali,  Mkoa huo unaendelea na programu maalum ya kuzungumza na madereva wa aina mbali mbali , ikiwemo wanaoendesha gari za watalii, baada ya kubaini kuwepo matukio ya ajali za mara kwa mara zinazojitokeza Mkoani humo.

Mapema, Mwenyekiti wa Kampuni ya ZK Venture Ltd, Wawekezaji wa Mradi wa Marijani Resort & SPA Amin Manji alisema ujio wa mradi huo unatokana na ari na juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali mwinyi za kuvutia Wawekezaji kote Duniani  kuja kuekeza Zanzibar.

Alisema Mradi wa Marijani Resort & SPA ni mradi wa hoteli ya Nyota tano, uliofanikishwa ujenzi wake kupitia Kampuni mbali mbali za Kizalendo, ukiwa na jumla ya vyumba 82 na maeneo mbali mbali ya utoaji huduma pamoja na kuwa na uwezo wa kuchukua wageni 104.

Alimpongeza Mwekezaji huyo kwa kutoa fursa  kwa wakulima wa Mwani kuendelea na shughuli  za kilimo hicho katika maeneo yao ya asili (mbele ya hoteli) pamoja na kuwapatia eneo maalum kwa ajili ya kuanikia mwani huo.

Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangalia namna ya kuwainua wakulima wa kilimo hicho cha mwani, kwa kigezo cha kutozwa kiwango kidogo cha bei, ikilinganishwa na  kazi ngumu ya kilimo hicho, sambamba na kuiomba Serikali kuwaondolea kero ya ukosefu wa maji safi na salama wananchi wa eneo hilo.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari, Ikulu Zanzibar.

January 06, 2022

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Translate »