Makamu wa Rais Mhe. Hemed amekagua Ujenzi wa Soko la Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini.

Makamu wa Rais Mhe. Hemed amekagua Ujenzi wa Soko la Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini.

Makamu wa Pili wa Rais Wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekagua maendeleo ya Ujenzi wa Miradi ya Masoko ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini yaliyopo Mkoa wa Mjini Magharib Unguja Akizungumza katika ziara yake hiyo Mhe. Hemed ameeleza kufurahiswa kwake baada ya kuona wasimamizi na wakandarasi wa ujenzi wa miradi hiyo ni wazawa wenye uzalendo

Makamu wa Pili wa Rais Wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekagua maendeleo ya Ujenzi wa Miradi ya Masoko ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini yaliyopo Mkoa wa Mjini Magharib Unguja

Akizungumza katika ziara yake hiyo Mhe. Hemed ameeleza kufurahiswa kwake baada ya kuona wasimamizi na wakandarasi wa ujenzi wa miradi hiyo ni wazawa wenye uzalendo wa kuitumikia Nchi yao.

Ameeleza kuwa ujenzi wa masoko hayo ni katika muendelezo wa kuwawekea ustawi wananchi kwa kuwasogezea huduma bora karibu na maeneo wanayoishi. Pia, ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Nane (8) inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambayo inakwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025 katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Mhe. Hemed amesema kukamilika kwa ujenzi wa miradi hiyo kutatatua changamoto ya wananchi kufuata huduma hiyo mbali na makaazi yao. Aidha, wafanyabiashara wataweza kufanya shuhuli zao katika masoko ya kisasa yenye ubora na viwango vya hali ya juu yatakayowawezesha wafanyabiashara hao kufanya kazi kwa uweledi mkubwa.

Amesema, anafahamu kuwa wakandarasi wanakabiliwa na changamoto mbali mbali lakini amewataka wasimamizi wa miradi hiyo changamoto hizo zisiwe sababu ya kukwamisha ujenzi huo. Aidha, amewaelekeza wasimamizi na wajenzi wa masoko hayo kuongeza kasi na juhudi ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ndani ya muda kwa mujibu wa mkataba.

Katika ziara yake hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, amevipongeza vikosi vya ulinzi na usalama ambavyo vimepewa dhamana ya kujenga masoko hayo pamoja na Wakala wa Majengo (ZBA) kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya na kusema kuwa ameridhishwa na utendaji kazi wao kwani hatua waliyofikia `ni nzuri ukilinganisha na mwezi uliopita alipotembelea miradi hiyo.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza ujenzi wa miradi mbali mbali Nchini na kuwataka kutoyazingatia maneno ya watu ambao wanabeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwani kumalizika kwa miradi hiyo kutawanufaisha wanzanzibari wote bila ya ubaguzi.

Amesema kuwa kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ni kuashiria kazi ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo imeanza, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kufanya kazi kwa bidii na kuachana na maneno yasiyo na faida kwa Taifa letu.

Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mhe. Massoud Ali Mohammed ameeleza kuwa yatakapokamilika masoko hayo, katika soko la mwanakwerekwe zaidi ya wafanyabiashara elfu nne (4,000) watanufaika, na katika soko la Jumbi na Chuini zaidi ya wafanyabiashara elfu nne na mia tano (4,500) watanufaika.

Mhe. Massoud amemuahidi Mhe. Hemed kuwa maagizo na miongozo anayowapatia Wizara itayatekeleza kwa haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu kwa maslahi mapana ya wananchi wa Zanzibar.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema kujengwa kwa masoko hayo katika Mkoa wa Mjini Magharibi kutazidi kufungua biashara ndani ya Mkoa na kumuomba Mhe. Makamu aridhie soko la Jumbi kuwa ndio kituo cha kupokea biashara kutoka ndani na nje ya Zanzibar.

Mhe. Kitwana amesema kuwa ujenzi huo unaendelea kutoa ajira kwa vijana wa kizanzibari na kuwanufaisha vijana wanaoendelea kujenga Taifa katika Vikosi mbali mbali vya SMZ ambavyo vimepewa dhamana ya kujenga masoko hayo.

Mshauri elekezi na msanifu majengo kutoka wakala wa Majengo (ZBA) ndugu Shadya Fauz Mohd, amesema wataendelea kusimamia na kujenga miradi yote kwa ubora na viwango vinavyokubalika ili kuyawezesha masoko hayo kutumika kwa muda mrefu.

Kwa upande wao wakandarasi wa miradi hiyo ambao ni kutoka vikosi vya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Chuo cha Mafunzo na Kikosi cha Zima Moto na Uokozi kwa pamoja wamemuahidi Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa wanafanya kazi kwa juhudi ili kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika kwa wakati ama kabla ya wakati uliopangwa na watazingatia ubora na viwango vya juu.

Ziara hiyo ni muendelezo wa ahadi ya Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa atatembelea miradi hiyo kila baada ya mwezi mmoja (01) ili kujionea maendeleo, kusikiliza maoni ya wakandarasi na kuharakisha kasi ya ujenzi huo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
13 Julai, 2023

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Translate »