WAZIRI MKUU AMEWAALIKA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA MBOLEA.

WAZIRI MKUU AMEWAALIKA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA MBOLEA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaalika wawekezaji waliobobea kwenye sekta ya mbolea ili waje kufungua viwanda vya mbolea nchini. Ametoa mwaliko huo leo (Alhamisi, Julai 27, 2023) wakati akizungumza kwenye mjadala uliohusu Uimarishaji wa Soko la Mbolea kama njia ya kuondoa njaa barani Afrika uliofanyika kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaalika wawekezaji waliobobea kwenye sekta ya mbolea ili waje kufungua viwanda vya mbolea nchini.

Ametoa mwaliko huo leo (Alhamisi, Julai 27, 2023) wakati akizungumza kwenye mjadala uliohusu Uimarishaji wa Soko la Mbolea kama njia ya kuondoa njaa barani Afrika uliofanyika kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg, Urusi.

Amesema uamuzi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuongeza bajeti ya kilimo una nia ya kuifanya Tanzania iwe eneo la uzalishaji la kulisha Afrika Mashariki, SADC na bara zima la Afrika. “Bado tuna changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa sababu ikikosekana inaathiri uzalishaji wa chakula.”

“Mbolea kwa sasa ndiyo msingi wa uzalishaji chakula. Uzalishaji wetu unatumia zaidi ya asilimia 80 na kwa maana hiyo tunalazimika kutumia fedha nyingi ili kuagiza mbolea kutoka nje na msisitizo wa sasa ni kuzalisha mbolea yetu.”

“Tunatumia fursa hii kutafuta marafiki ambao wako tayari kuja kuwekeza kwenye mbolea. Mahitaji yetu ni zaidi ya tani 800,000 wakati uzalishaji wetu ni tani 200,000. Tumeshapata kiwanda ambacho kinazalisha mbolea na sasa wameshafikisha tani 400,000 na wanalenga kufikia tani 800,000 lakini hatuwezi kuetegemea kiwanda kimoja peke yake,” amesema.

Amesema Tanzania ina rasilmali ya gesi ambayo inaweza kutumika kutengeneza mbolea ukiacha zile za kawaida za wanyama. “Tukifanikiwa kuongeza uzalishaji wa mbolea, tutakuwa na nafasi ya kuzalisha chakula zaidi. Jukwaa hili ni nafasi pekee ya kualika wawekezaji waliobobea kwenye maeneo kama haya,” amesisitiza.

Mapema, Waziri Mkuu alishiriki Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na Kibinadamu lililofunguliwa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg, Urusi.

Jukwaa hilo ambalo limehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Umoja wa Afrika wakiwemo wa Uganda, Msumbiji, Zimbabwe, Sudan, limehusisha pia Mawaziri, wakuu wa Mashirika ya Kikanda, Taasisi na Mashirika ya kiserikali kutoka Urusi na Afrika.

Jukwaa hilo linaenda sambamba na maonesho ya kimataifa ya bidhaa na huduma mbalimbali kutoka Urusi na Afrika pamoja na majukwaa ya majadiliano (side meetings) zaidi ya 30 ambayo yanahususu mada mbalimbali zikiwemo za masuala ya vijana, kilimo, afya, elimu, masuala ya kibinadamu.

Baadhi Mawaziri na Makatibu Wakuu na wakuu wa taasisi kutoka Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanashiriki majukwaa hayo ya majadiliano.

Maudhui makuu ya jukwaa hilo linalotarajiwa kutoa fursa kwa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kushirikiana na Urusi kukuza uchumi, kutafuta ushirikiano wa kibiashara na kushughulikia changamoto za kimaendeleo yanahusu Uchumi Mpya wa Dunia (the New Global Economy); Usalama Jumuishi (Integrated Security); Sayansi na Teknolojia (Science and Technology); na Masuala ya Kibinadamu na Kijamii (Humanitarian Issues).

Kesho Waziri Mkuu anatarajiwa kushiriki ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, JULAI 27, 2023.

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Latest Posts

Top Authors

Most Commented

Featured Videos

Translate »