Waziri Mkuu Majaliwa amezindua nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Muungano.

Waziri Mkuu Majaliwa amezindua nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Muungano.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote, Bara na Visiwani waendelee kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.  “Kwa heshima na taadhima nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassanpamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wao makini ambao umekuwa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizindua nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Kambarage, Hazina jijini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na washiriki katika uzinduzi wa nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Kambarage, Hazina jijini Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na washiriki katika uzinduzi wa nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Kambarage, Hazina jijini Dodoma.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote, Bara na Visiwani waendelee kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 

“Kwa heshima na taadhima nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassanpamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wao makini ambao umekuwa chachu ya kudumisha muungano wetu.”

Ameyasema hayo leo (Aprili 8, 2024) wakati akizindua nembo na kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano. “Muungano huu ni tunu adimu na adhimu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Hivyo basi kila mmoja awe mlinzi.“

Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano yamebeba kaulimbiu isemayo, “Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’ Tumeshikamana na Tumeimarika, kwa Maendeleo ya Taifa Letu’’.  

Amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia muungano wao kutimiza miaka 60. “Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla.“ 

“Kama ulivyo msemo wa Kiswahili Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, muungano wetu umefanya Tanzania liwe Taifa lenye utulivu, mshikamano, nguvu na mfano kwa mataifa mengi Barani Afrika na duniani kwa ujumla.“ 

Waziri Mkuu amesema kilele cha sherehe za muungano kitafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam, hivyo ametoa wito kwa wananchi wote wa pande mbili za muungano wajitokeze kwa wingi ili kushuhudia maadhimisho hayo.

“Wananchi wote tumieni maadhimisho haya kutafakari tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi tangu muungano uliopoasisiwa mwaka 1964. Kaulimbiu ya maadhimisho haya ituongoze katika tafakuri hiyo ili kwa pamoja tuendelee kuulinda na kuutetea muungano wetu.“

Ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi zinazotoa elimu, ziendelee kufundisha mada kuhusu muungano wetu kuanzia elimu ya awali ili watoto na vijana waufahamu na wawe walinzi na hatimaye wawe vinara katika kuundeleza.      

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema nchi itaendesha uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, hivyo ametoa rai kwa wapigakura wote wahakikishe wanajiridhisha na kushiriki taratibu za kuwafanya kuwa na sifa za kushiriki kuchagua viongozi wenye uwezo na wenye nia njema na Muungano. 

Waziri Mkuu ametoa ratiba ya matukio yatakayofanyika kuwa ni pamoja na uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano utakaofanyika Zanzibar tarehe 14 Aprili, 2024 pamoja na uzinduzi wa Maonesho ya Biashara ya Taasisi za Muungano. Mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt, Hussein Ali Mwinyi.

Amesema kutakuwa na Maonesho ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara yatakayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Abdulla. 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Maadhimisho haya yataambatana na uzinduzi wa miradi ya maendeleo utakaoanza tarehe 15 Aprili na kuendelea hadi mwisho wa Mei, 2024.

“Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango ataliongoza Taifa katika siku maalum ya maombi na dua kwa Taifa itakayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma tarehe 22 Aprili, 2024.  Viongozi wa Kitaifa wa Dini zote watahudhuria katika ibada hiyo.” 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema wilaya zote hapa nchini zitaandaa maombi kwa Taifa yatakayofanyika katika siku hiyo. “Nisisitize kila Mkuu wa Wilaya aanze kufanya uratibu ili nchi yetu yote ishiriki katika maombi na dua hizo.”

Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ataliongoza Taifa katika kuzindua kitabu cha Historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais, shughuli itakayofanyika 23 Aprili na tarehe 24 Aprili, 2024 atatunuku Nishani za Taifa kwa watu mbalimbali, shughuli zote zitakafanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam. 

“Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu atakuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Muungano litakalofanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Jijini Dar es Salaam tarehe 25 Aprili, 2024.”

Waziri Mkuu amesema kuwa tarehe 26 Aprili, 2024, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ataliongoza Taifa katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano yatakayofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam.

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Translate »