HOTUBA YA WAZIRI MKUU MAJALIWA WAKATI AKIAHIRISHA MKUTANO WA BUNGE LEO.

HOTUBA YA WAZIRI MKUU MAJALIWA WAKATI AKIAHIRISHA MKUTANO WA BUNGE LEO.

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WAJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI AKIAHIRISHA MKUTANO WA5 WA BUNGE LA 12 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TAREHE 12 NOVEMBA, 2021 JIJINI DODOMA UTANGULIZIShukrani Mheshimiwa Spika, leo tunafikia tamati ya mkutano wa tano wa Bunge lakotukufu ulioanza tarehe 2 Novemba, 2021. Kwa msingi huo,

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI AKIAHIRISHA MKUTANO WA
5 WA BUNGE LA 12 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TAREHE 12

NOVEMBA, 2021 JIJINI DODOMA

UTANGULIZI
Shukrani

  1. Mheshimiwa Spika, leo tunafikia tamati ya mkutano wa tano wa Bunge lako
    tukufu ulioanza tarehe 2 Novemba, 2021. Kwa msingi huo, tunayo kila sababu ya
    kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli
    zote zilizopangwa kwenye mkutano huu tukiwa buheri wa afya.
  2. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa weledi, busara na uwezo mkubwa
    uliouonesha katika kuliongoza Bunge hili umekuwa chachu ya kuhitimisha shughuli za
    Bunge hili kwa mafanikio makubwa. Hivyo basi, nitakuwa mchoyo wa fadhila iwapo
    sitokushukuru wewe binafsi kwa kuendelea kuliongoza Bunge hili kwa umahiri mkubwa.
  3. Mheshimiwa Spika, vilevile, niwashukuru Mheshimiwa Naibu Spika na
    Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge kwa kuendelea kukusaidia kikamilifu katika kutekeleza
    majukumu ya kuliongoza Bunge letu tukufu.
  4. Mheshimiwa Spika, ninawashukuru pia, Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa
    kazi nzuri, michango, maoni na ushauri tulioupokea katika mkutano huu. Serikali kwa
    upande wake imepokea michango yenu yenye nia ya kujenga na kuimarisha utendaji wa
    Serikali na inaahidi kuifanyia kazi.
    Salamu za Pole
  5. Mheshimiwa Spika, tarehe 27 Septemba 2021, Bunge lako tukufu lilipata pigo
    kubwa kwa kuondokewa na Mheshimiwa William Tate Ole Nasha, aliyekuwa Mbunge wa
    Jimbo la Ngorongoro na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji). Ninatoa
    pole kwako Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Ngorongoro, ndugu, jamaa na
    marafiki wote walioguswa na msiba huo.
  6. Mheshimiwa Spika, halikadhalika, katika kipindi hicho cha Septemba hadi
    Novemba 2021, wapo Watanzania wenzetu waliopatwa na masahibu mbalimbali ikiwemo
    ajali za barabarani ambazo zimegharimu maisha ya watu, majeruhi na kusababisha
    uharibifu wa mali. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema na awaponye
    majeruhi wote. Amin!
    Salamu za Pongezi
  7. Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Septemba, 2021 vilevile, Mheshimiwa Samia
    Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya mabadiliko katika
    Baraza la Mawaziri ambapo alimteua Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb.)
    kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb.) kuwa
    Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Mheshimiwa January Yusuf
    Makamba (Mb.) kuwa Waziri wa Nishati; Mheshimiwa Prof. Makame Mnyaa Mbarawa kuwa
    Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mheshimiwa Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa
    Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

2

  1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwatakia heri katika
    kutimiza majukumu yao viongozi wote walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali.
    Niwakumbushe tu kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
    Muungano wa Tanzania anayo matarajio makubwa kutoka kwenu katika kutimiza shauku
    ya Watanzania kuona mafanikio kwenye sekta mnazozisimamia.
    SHUGHULI ZA BUNGE
    Maswali na Majibu
  2. Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu jumla ya maswali 98 ya msingi na
    mengine 247 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.
    Aidha, maswali nane ya papo kwa papo yalielekezwa kwa Waziri Mkuu na kujibiwa.
    Taarifa za Kamati
  3. Mheshimiwa Spika, Bunge lilipokea na kujadili Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya
    Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni
    kwenye mkutano wa tatu, tarehe 9 Aprili, 2021 na mkutano wa nne, tarehe 7 Septemba,
    2021 pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009.
    Miswada ya Sheria
  4. Mheshimiwa Spika, tunapohitimisha mkutano huu, tumeweza kukamilisha
    mjadala wa miswada miwili ya sheria iliyowasilishwa katika Bunge lako tukufu. Muswada
    wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 6 wa Mwaka 2021 ulisomwa kwa
    hatua zake zote na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 7 wa
    Mwaka 2021 ulisomwa kwa mara ya kwanza.
  5. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa katika mkutano wa 4 wa Bunge la 12,
    Serikali iliahidi kuwasilisha Muswada wa Sheria kuhusu Bima ya Afya kwa Wote. Serikali
    inatoa umuhimu mkubwa kwenye suala hili sambamba na kuhakikisha masuala yote ya
    kisera, kisheria na kibajeti yanatazamwa kwa kina. Hatua muhimu za awali zimekamilika
    na sasa tunawashirikisha wadau wengi zaidi ili kutengeneza mfumo ambao hautokuwa na
    changamoto nyingi.
  6. Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuona utekelezaji wake unaanza mwaka
    ujao wa fedha 2022/2023 ili kila mwananchi awe na uhakika wa kupata matibabu kila
    itakapolazimu. Hivyo basi, nitoe maelekezo kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
    Jinsia, Wazee na Watoto ishirikiane na wadau wote muhimu katika kuhakikisha Muswada
    wa Sheria kuhusu Bima ya Afya kwa Wote unakamilika kwa wakati ili kukidhi malengo ya
    Serikali na matarajio ya wananchi.
    MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA
    UVIKO-19
  7. Mheshimiwa Spika, tarehe 10 Oktoba 2021, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi
    wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 jijini Dodoma.
  8. Mheshimiwa Spika, mpango huo uliotokana na mkopo nafuu wa takriban shilingi
    trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) unaolenga kuiwezesha Jamhuri
    ya Muungano wa Tanzania kukabiliana na athari za UVIKO19 katika uchumi na maisha ya
    Watanzania kwa ujumla.

3

  1. Mheshimiwa Spika, sekta zitakazonufaika na mpango huo ni Maji (shilingi bilioni
    139.4), Elimu (shilingi bilioni 368.9), Afya (shilingi bilioni 466.9), Utalii (shilingi bilioni
    90.2), Jamii inayoishi kwenye mazingira magumu (shilingi bilioni 5.5) zikiwemo kaya
    maskini na Kundi la Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu (shilingi bilioni 5). Aidha,
    shilingi bilioni 231 zimeelekezwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na shilingi bilioni 5 ni
    kwa ajili ya shughuli za uratibu.
  2. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango huo utaimarisha miundombinu ya
    afya, elimu, maji, utalii, maeneo ya biashara za wajasiriamali wadogo, uwezeshaji wa
    makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na kaya masikini. Kwa
    upande mwingine, mpango huo utaimarisha upatikanaji sambamba na kusogeza huduma
    za jamii karibu na wananchi. Hii inatokana na ukweli kwamba uwekezaji mkubwa
    umefanywa kwenye eneo la vifaa hususan mitambo ya uchimbaji wa maji na visima na
    vifaa tiba.
  3. Mheshimiwa Spika, fedha hizo za dharura zinapaswa kutumika ndani ya kipindi
    cha miezi tisa hususan mwaka huu wa fedha 2021/2022. Kwa kuzingatia hilo, Serikali
    tayari imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha matarajio ya Mheshimiwa Rais katika
    utekelezaji wa mpango huo yanafikiwa. Baadhi ya hatua hizo ni kama ifuatavyo: –
    Moja: Kuunda kamati za uratibu kwa ngazi ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kwa kila
    mkoa na Halmashauri ambapo kamati hizi zimejumuisha viongozi kutoka
    ngazi ya Wizara, Wakuu wa Idara na Vitengo watakaokuwa na jukumu la
    kufuatilia utekelezaji wa miradi yote iliyoainishwa;

Mbili: Kuandaa utaratibu wa manunuzi ya pamoja kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI
kwa vifaa vya huduma za dharura, ICU, X-Ray, magari ya kubebea
wagonjwa ambayo yatagawiwa katika Halmashauri zote na Magari ya uratibu
wa huduma za afya katika Mikoa yote;

Tatu: Kuwaelekeza Wakuu wote wa Mikoa, Wilaya na Watendaji wa Halmashauri
kuepuka safari zisizo za lazima katika kipindi chote cha utekelezaji wa
Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-
19; na

Nne: Kuhamasisha wananchi na wawakilishi wao kushiriki ipasavyo katika ujenzi
wa miradi inayoendelea kwenye maeneo yao na kutoa taarifa endapo
watabaini uwepo wa viashiria vya ubadhirifu wa fedha au vifaa vya miradi.

  1. Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo na katika kuhakikisha uwepo wa
    thamani ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo, ninaelekeza
    masuala yafuatayo kwa wote wanaohusika: –
    Mosi: Viongozi na Watendaji wasimamie na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa
    miradi yote iliyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa
    Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19;

Pili: Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
wahakikishe hadi kufikia Januari 2022, madarasa yote kwa ajili ya wanafunzi
wa kidato cha kwanza yawe yamekamilika;

4

Tatu: Wakuu wa Mikoa wahakikishe wanasimamia ipasavyo mipango ya usimamizi
kupitia Sekretarieti za Mikoa. Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa
zihakikishe zinafuatilia utekelezaji huo sambamba na kutembelea maeneo
husika ili kujiridhisha na thamani ya fedha zilizotolewa na ujenzi uliofanyika;
na

Nne: Wakuu wa Mikoa wahakikishe Sekretarieti husika zinawashirikisha wananchi
na wawakilishi wao katika kutekeleza miradi iliyopo kwenye Mpango wa
Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.

  1. Mheshimiwa Spika, natambua kwamba ilikuwepo hofu kuhusu kupatikana na
    wakati mwingine kupanda kwa bei ya baadhi ya vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji, bati,
    nondo, marumaru, vifaa vya umeme n.k.
  2. Mheshimiwa Spika, katika hatua ya kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali
    ilikutana na wazalishaji na hata kutembelea baadhi ya maeneo ya uzalishaji ili kujiridhisha
    na hali ilivyo kwa upande wa bidhaa hizo. Nitumie fursa hii kulihakikishia Bunge lako
    tukufu kwamba wazalishaji wetu wamejipanga vizuri kiuzalishaji na hatutarajii uhaba au
    mtikisiko wa bei kwa bidhaa lengwa. Niendelee kusisitiza kuwa Wizara ya Viwanda na
    Biashara isimamie na ifuatilie mwenendo wa bei ya bidhaa hizo kutoka viwandani hadi kwa
    walaji.
    MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA
    2022/2023
  3. Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu lilipokea, kujadili, kushauri na kupitisha
    Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali
    pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha
    2022/2023.
  4. Mheshimiwa Spika, katika kukidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
    wa Tanzania Ibara ya 63(3)(c) na Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu Ibara ya 11,
    hoja hiyo ilijadiliwa kwa siku tano kuanzia tarehe 3 Novemba 2021 na kuhitimishwa tarehe
    09 Novemba 2021.
  5. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Mwigulu
    Lameck Nchemba (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango na Mheshimiwa Mhandisi Hamad
    Yussuf Masauni (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kwa maelezo mazuri ya
    ufafanuzi waliyotoa wakati wa kuhitimisha hoja hiyo.
  6. Mheshimiwa Spika, vilevile, niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa mchango
    mzuri waliotoa wakati wa mjadala wa hoja hiyo. Katika mjadala huo, tulipata darasa zuri
    kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wametupa uelewa mpana utakaotusaidia
    kuboresha utekelezaji wa mpango huo kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi yetu.
  7. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2022/2023 ni
    wa kwanza kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu
    Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

5

  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, mpango huo utaendelea
    kutekeleza maeneo mahsusi ya kipaumbele ambayo ni: (i) kuchochea uchumi shindani na
    shirikishi; (ii) kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; (iii) kukuza
    biashara na uwekezaji; (iv) kuchochea maendeleo ya watu na (v) kuendeleza rasilimali
    watu. 
  2. Mheshimiwa Spika, sambamba na mapendekezo ya mpango huo, pia,
    uliwasilishwa Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2022/2023.
    Hivyo, nami nitumie fursa hii kusisitiza baadhi ya mambo muhimu ambayo hayanabudi
    kuzingatiwa kikamilifu na viongozi na watendaji wote wakati wa maandalizi na utekelezaji
    wa bajeti ya mwaka 2022/2023 kama ifuatavyo: –
    Moja: Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani. Hili ni miongoni mwa maeneo yaliyoibua
    hoja kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. Hivyo, nisisitize kuwa Wizara ya
    Fedha ishirikiane na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuimarisha matumizi ya vifaa vya
    kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Serikali;

Mbili: Riba kubwa za mikopo kutoka kwenye mabenki ya biashara na
taasisi za fedha: Serikali imekuwa ikichukua hatua madhubuti kupitia Benki
Kuu ya Tanzania ikiwemo kupunguza kiwango cha akiba kinachowekwa na
mabenki katika Benki Kuu, kulegeza masharti ya uanzishwaji wa ofisi za
wakala wa mabenki, kushusha riba inayolipwa kwa akaunti za fedha za
mitandao pamoja na kutenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya mikopo kwa
mabenki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia tatu ili mabenki na taasisi hizo
zitoe mikopo kwa riba isiyozidi asilimia 10. Mheshimiwa Spika, hatua hizo
zinalenga kupunguza kiwango cha riba kwenye mikopo ya mabenki ya
kibiashara na taasisi za fedha, kupunguza riba katika shughuli za kilimo kwa
kiwango kisichozidi asilimia 10 na kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa
sekta binafsi ili kuchechemua shughuli za kiuchumi. Licha ya hatua hizo, bado
kumekuwa na changamoto ya kutoshuka kwa kiwango cha riba kinachotozwa
na mabenki na taasisi za fedha. Kwa mantiki hiyo, ninaiagiza Wizara ya Fedha
na Mipango ikutane na taasisi za fedha nchini kuona namna wanavyoweza
kupunguza riba kubwa kwenye mikopo wanayotoa hususan kwa makundi ya
wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo;

Tatu: Kuwawezesha Wakandarasi wa Ndani: Wizara ya Fedha shirikianeni na
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi katika kuhakikisha inatekeleza vema Mpango wa
Serikali wa kuwajengea uwezo na kuwawezesha wakandarasi wa ndani sanjari
na kuendelea kulipa madeni ya wazabuni kwa wakati;

Nne: Mafao ya Wastaafu. Katika hili namuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu) ashirikiane na
Waziri wa Fedha na Mipango kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa
mafao ya wastaafu kwa wakati inaondoka na wastaafu walipwe kwa wakati;
Tano: Kudhibiti Matumizi na Kupunguza Gharama: Maafisa Masuuli endeleeni
kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya Serikali yasiyokuwa ya lazima na
kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali zinazojiendesha kibiashara, zinapata faida
na kuacha kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu; na

Sita: Kudhibiti Ongezeko la Madeni ya Serikali: Maafisa Masuuli wote
hakikisheni madai ya watoa huduma yote yanahakikiwa na kuingizwa kwenye

6

hesabu za fungu husika, kutoingia mikataba ya miradi mipya bila kuwa na
uhakika wa upatikanaji fedha; na kuzingatia matumizi ya hati za ununuzi
zinazotolewa kwenye mfumo wa malipo ili kudhibiti ulimbikizaji wa madeni.

  1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha viongozi na watendaji wote
    Serikalini kuzingatia kikamilifu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka
    2022/2023 ili kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita.
    KILIMO
    Utabiri wa Hali ya Hewa na Uhakika wa Chakula Nchini
  2. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa kilimo wa
    mwaka 2020/2021 ulikuwa mzuri. Katika msimu huo uzalishaji ulifikia tani milioni 18.42
    ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 14.79. Kwa lugha nyingine tuna ziada ya tani
    milioni 3.63.
  3. Mheshimiwa Spika, hivi sasa tupo katika msimu wa kilimo 2021/2022 ambapo
    baadhi ya maeneo ya nchi yetu yameanza kupata mvua za vuli. Hata hivyo, taarifa ya
    Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania iliyotolewa Septemba na Oktoba 2021 imeonesha
    kuwa viwango vya unyeshaji mvua katika msimu huu wa kilimo vitakuwa vya wastani
    katika baadhi ya maeneo hali imbayo itaathiri uzalishaji wa baadhi ya mazao kama
    mpunga na mahindi kutokana na vipindi virefu vya ukame.
  4. Mheshimiwa Spika, Serikali imeshachukua hatua mahsusi ili kukabiliana na
    athari zinazoweza kujitokeza kutokana na upungufu wa mvua. Hatua hizo ni pamoja na
    Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuendelea kununua chakula na kuhifadhi na
    kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ukuaji wa mazao shambani sambamba na kufanya
    tathmini ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu 2021/2022.
    Hali ya Upatikanaji wa Mbolea
  5. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa matumizi ya mbolea, mbegu bora na
    viuatilifu ni muhimu katika kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo. Serikali
    imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi katika kuzalisha, kuagiza na kusambaza pembejeo
    kwa wakulima kulingana na mahitaji na ikolojia ya kilimo. Serikali imekuwa ikichukua
    hatua kadhaa katika kuhakikisha pembejeo za kilimo hususan mbolea zinapatikana kwa
    bei nafuu, kwa wakati lakini pia kwa kiwango cha kutosha. Miongoni mwa hatua hizo ni
    matumizi ya mifumo ya upatikanaji wa mbolea kupitia uzalishaji ndani ya nchi na uagizaji
    wa mbolea kwa pamoja kutoka nje ya nchi.
  6. Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2021/2022 makisio yanaonesha kuwa
    mahitaji ya mbolea ni tani 698,260 na wastani wa matumizi kwa mwaka ni tani 430,000.
    Hata hivyo, hadi kufikia Oktoba 2021 upatikanaji wa mbolea ulikuwa ni tani 333,903 sawa
    na asilimia 48 ya mahitaji.
  7. Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa mbolea duniani kote imeathiriwa na
    uwepo wa UVIKO 19. Hali hiyo, imesababisha kusimama kwa uzalishaji, baadhi ya nchi
    kusitisha uuzaji wa mbolea nje, kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na upungufu wa
    malighafi za kutengeneza mbolea kutokana na baadhi ya nchi kufunga mipaka yake na
    hivyo kusababisha ongezeko la mahitaji na bei ya mbolea.

7

  1. Mheshimiwa Spika, kutokana na kusuasua kwa uagizaji wa mbolea na ongezeko
    la bei kwa takribani asilimia 96 ikilinganishwa na bei ya mwaka jana, Serikali imechukua
    hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo kama ifuatavyo:-
    Moja: kuwasiliana moja kwa moja na wazalishaji wa mbolea katika nchi rafiki ili

kupata mbolea kwa gharama nafuu;

Mbili: Kuruhusu wafanyabiashara kuingiza mbolea nchini bila kutumia zabuni za
mfumo wa ununuzi wa pamoja na kuuza kwa bei ya ushindani. Hatua hii
imesaidia kuongeza kiwango cha mbolea kilichoingizwa nchini kati ya Julai na
Oktoba 2021. Katika kipindi hicho, tani 48,400 za mbolea ya urea ziliingizwa
nchini ikilinganishwa na tani 33,948 zilinunuliwa kwa zabuni ya mfumo wa
pamoja msimu wa 2020/2021;

Tatu: Kuhamasisha matumizi ya mbolea mbadala wa DAP na Urea kama vile NPK,
NPS, NPSZinc, Nafaka+ ya Minjingu, mbolea za asili, chokaa na mbolea ya
Fomi Imbura inayozalishwa na Kiwanda cha Fomi cha Burundi;

Nne: Kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya ndani vya kuzalisha mbolea ikiwa ni
sehemu ya suluhisho la muda mrefu. Tayari ujenzi wa kiwanda cha Kampuni
ya Itracom Fertilizers Limited kutoka Burundi umeanza na utakapokamilika
kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka.
Kadhalika, kuongeza uzalishaji katika kiwanda cha Minjingu ili kizalishe sawa
na uwezo wake wa tani 100,000 kwa mwaka;

Tano: Kukamilisha mazungumzo na Serikali ya Burundi kuhusu kununua mbolea ya
Fomi Imbura. Nitoe wito kwa Watanzania kuzitumia aina nyingine za mbolea
kwani zinatumika kwa mafanikio kwa nchi jirani na hata baadhi ya maeneo
ya Tanzania;

Sita: Serikali kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imekwishaagiza tani
20,000 za mbolea ya kupandia (DAP) na tani 60,000 za mbolea ya kukuzia
(Urea). Mbolea hii itauzwa kwa gharama nafuu ambayo inalingana na uwezo
wa wakulima wetu nchini; na

Saba: Kukamilisha utafiti wa afya ya udongo katika mikoa ya Pwani, Dar es
Salaam, Mtwara, Lindi, Tanga, Ruvuma, Tabora na Kigoma kwa lengo la
kuwezesha viwanda vya mbolea hususan vilivyoko nchini kuzalisha mbolea
kulingana na afya ya udongo sambamba na matumizi sahihi ya mbolea.

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa taarifa muhimu na elimu kwa umma
    kuhusu hali ya hewa na bei ya mbolea duniani. Niwaagize Wakuu wa Mikoa hasa ya
    mipakani wasizuie mbolea kuingizwa nchini kwa sababu bado uhitaji ni mkubwa na pia
    wasiruhusu mbolea iuzwe nje ya nchi. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu
    mnaporudi kwenye majimbo yenu mtoe elimu kwa wananchi kuhusu changamoto ya bei
    ya mbolea na kuhamasisha matumizi ya mbolea mbadala zinazopatikana kwa bei nafuu.
    UMWAGILIAJI

8

  1. Mheshimiwa Spika, kwa sasa Taifa letu lina mfumo wa umwagiliaji wenye
    ukubwa wa hekta 600,000 ambao mtandao huo pamoja na uwepo wake haufanyi kazi kwa
    asilimia 100. Kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM; lengo la Serikali ni kuhakikisha
    sekta ya umwagiliaji inakuwa na miundombinu ya umwagiliaji yenye ukubwa wa hekta
    milioni 1.2 ifikapo mwaka 2025.
    Ninawaagiza Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha kukaa pamoja na kufanya mambo
    yafuatayo kwenye mpango wa 2022/23 na bajeti ya mwaka ujao wa fedha:-
    (1) Kuhakikisha kila Mkoa na Wilaya kuna Ofisi ya Tume ya Umwagiliaji na vitendea kazi
    na wahandisi wenye sifa.
    (2) Kuhakikisha wahandisi wa umwagiliaji waliopo kwenye Halmashauri na wahandisi wa
    Tume ya Umwagiliaji wanafanya kazi chini ya Ofisi za Tume ya Umwagiliaji.
    (3) Kufanya usanifu wa miundombinu ya umwagiliaji kwa maeneo mapya ili kujenga
    skimu mpya zenye ukubwa wa hekta 600,000 kufikia mwaka 2025.
    (4) Kufanya tathmini ya kina yaskimu za umwagiliaji zilizopo na kuzikarabati ili ziweze
    kufikia ubora na ufanisi unaotakiwa.
    (5) Kutenga fedha kupitia bajeti ya Wizara kwa ajili ya kununua vifaa na mitambo
    ambayo itakuwa katika kanda nane za kilimo ili zitumike kutunza, kurekebisha na
    kujenga mabwawa madogo madogo kwenye maeneo ambayo wakati wa masika maji
    mengi hupotea.
    (6) Wizara ya Fedha kwa pamoja na Wizara ya Kilimo andaeni miradi ya kielelezo ya
    umwagiliaji, maghala na uwekezaji kwenye maeneo ya uhifadhi wa mazao ya nafaka
    na mazao ya bustani (Horticulture).
    UMEME VIJIJINI
  2. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge
    wakati wa mkutano huu ni pamoja na suala la kuharakisha upatikanaji wa umeme vijijini.
    Kama alivyoeleza Waziri wa Fedha na Mipango alipokuwa akiwasilisha Mapendekezo ya
    Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2022/2023, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji
    wa umeme hususan maeneo ya vijijini.
  3. Mheshimiwa Spika, hadi sasa jumla ya vijiji 10,361 kati ya vijiji 12,317 vya
    Tanzania Bara sawa na asilimia 84.12 vimeunganishiwa umeme. Lengo la Serikali ni
    kuhakikisha hadi kufikia Desemba 2022 vijiji 1,956 vilivyosalia vinapata umeme kupitia
    Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ulioanza kutekelezwa
    Julai, mwaka huu. Gharama za mradi huu ni shilingi trilioni 1.24.
  4. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha maeneo yote ya mijini na vijijini yanapata
    umeme wa kutosha, nafuu na uhakika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji
    na usambazaji umeme maeneo mbalimbali nchini. Baadhi ya miradi ya kimkakati ya
    uzalishaji umeme ni mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (MW 2,115)
    ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 55.6 na mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa
    Rusumo (MW 80) uliofikia asilimia 81.2.

9

  1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imekamilisha mradi wa njia ya kusafirisha
    umeme (KV 220) kutoka Bulyanhulu hadi Geita wenye urefu wa kilomita 55. Miradi
    mingine ya kusafirisha umeme inayoendelea kutekelezwa ni kutoka Rusumo kwenda
    Nyakanazi kupitia Benaco (KV220), Tabora kupitia Urambo – Nguruka hadi Kidahwe (KV
    132) na Tabora hadi Katavi kupitia Ipole na Inyonga (KV132). Aidha, Serikali inaendelea
    na maandalizi ya Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa kV 400 kutoka Iringa –
    Mbeya – Tunduma hadi Sumbawanga na mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa KV 400
    kutoka Sumbawanga – Mpanda hadi Kigoma.
  2. Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa miradi hiyo ya uzalishaji na usambazaji
    umeme kutawezesha maeneo yote nchini kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa na hivyo
    kupata huduma ya uhakika ya umeme. Jukumu la TANESCO ni kuhakikisha usambazaji
    umeme kwenye makazi ya watu unafanywa kwa kasi ili lengo la Mheshimiwa Rais la kuona
    kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme liweze kutimia.
    MIKOPO YA ELIMU YA JUU
  3. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu
    kwa kuongeza kiwango cha fedha za kugharamia mikopo ya elimu ya juu na hivyo
    kuongeza idadi ya wanufaika. Kwa mfano, katika mwaka wa masomo 2021/2022, Serikali
    imetenga shilingi bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ikilinganishwa na shilingi
    bilioni 464 zilizotumika mwaka 2020/2021. Vilevile, idadi ya wanufaika imeongezeka
    kutoka 149,398 mwaka 2020/2021 hadi 170,000 mwaka 2021/2022.
  4. Mheshimiwa Spika, upangaji wa mikopo unaendelea kwa kuzingatia utaratibu,
    sifa na vigezo vilivyowekwa. Kwa msingi huo, ninaelekeza kama ifuatavyo: –
    Moja: Waombaji wote wa mkopo hakikisheni mnakamilisha taratibu za uombaji wa
    mkopo ikiwa ni pamoja na kujisajili kwenye mfumo wa maombi ya mikopo
    (OLAMS) kwa wakati. Vilevile, hakikisheni mnawasilisha taarifa sahihi ili
    muweze kuhudumiwa bila bughudha;

Mbili: Baada ya kufunguliwa kwa dirisha la rufaa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
harakisheni mchakato wa rufaa ili wanafunzi husika waweze kupata stahiki
zao, watulie na kuendelea na masomo yao kama kawaida;

Tatu: Mamlaka zote za vyuo vikuu vyenye wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya
elimu ya juu kamilisheni na kuwasilisha taarifa za wanafunzi ili kuiwezesha
Bodi ya Mikopo kuwapangia mikopo na kuhakikisha wanapokea stahili zao
kwa wakati na kupunguza usumbufu usiokuwa wa lazima.

  1. Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio yaliyopatikana katika utoaji mikopo ya
    elimu ya juu, Serikali imepokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwemo
    Waheshimiwa Wabunge kuhusu kuboreshwa kwa mfumo wa sasa wa mikopo ya elimu ya
    juu. Maoni hayo ni pamoja kuanzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi
    wanaosoma katika vyuo vya elimu ya kati.
  2. Mheshimiwa Spika, maoni mengine ni kutoa ruzuku badala mikopo kwa
    wanafunzi wanaosomea shahada na stahashada zenye uhitaji mkubwa kitaifa na katika
    uzalishaji, na wale wanaotoka katika makundi yenye mahitaji maalum; lakini pia kufanya
    mapitio ya vipengele vya mikopo ili kuangalia uwezekano wa kuainisha vipengele vya

10

kukopeshwa na vinavyoweza kutolewa kama ruzuku kati ya gharama za ada za mafunzo
na zile za mahitaji mengineyo.

  1. Mheshimiwa Spika, ninaielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanya
    upya mapitio ya mfumo wa utoaji mikopo ili kuzingatia maoni ya wadau na uzoefu wa
    miaka iliyopita na ije na mapendekezo kuhusu mfumo bora utakaotatua changamoto za
    sasa sambamba na kuimarisha kasi ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu.
    BANDARI
  2. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa ya bandari
    zetu zilizopo kwenye Bahari ya Hindi na maziwa makuu ya Tanganyika, Victoria na Nyasa.
    Maboresho hayo, yanalenga kuongeza uwezo wa bandari zetu katika kuhudumia meli
    hususan za shehena na hivyo, kumudu ushindani wa kibiashara sambamba na kutumia
    vema fursa ya kijiografia katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
    Bandari ya Dar es Salaam
  3. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa uboreshaji wa bandari
    ya Dar es Salaam wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 421 umefikia asilimia 99 na
    unatarajiwa kukamilika mwaka huu wa fedha 2021/2022. Kukamilika kwa mradi huu,
    kutaongeza uwezo wa bandari ya Dar es Salaam wa kuhudumia meli kubwa zinazohitaji
    kina kirefu zaidi kuliko ilivyo sasa, zenye urefu wa hadi mita 305 na uwezo wa kubeba
    makasha kati ya 7,000 hadi 8,000.
  4. Mheshimiwa Spika, vilevile, uwezo wa bandari hiyo wa kuhudumia shehena
    kubwa ya mizigo utaongezeka kutoka tani milioni 16 za sasa hadi tani milioni 25. Hivyo,
    kuongeza mapato ya Taifa na kumudu ushindani na bandari nyingine za ukanda wa Bahari
    ya Hindi kama vile Mombasa, Maputo, Beira, Nacala na Durban.
  5. Mheshimiwa Spika, hivi sasa bandari ya Dar es Salaam imeanza kupokea meli
    kubwa zenye uwezo wa kubeba hadi magari 6,000 pamoja na kuongeza uwezo wa
    kuhudumia meli kubwa hadi tatu za aina moja ya shehena kwa wakati mmoja.
    Bandari ya Tanga
  6. Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Bandari ya Tanga
    ambayo ilihusisha uongezaji wa kina cha lango la bandari kutoka mita 4 hadi mita 13 na
    ujenzi wa gati mbili kwenye kina kirefu umekamilika. Katika mwaka 2020/2021, mradi huo
    uligharimu shilingi bilioni 20.41.
  7. Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya uboreshaji wa bandari hiyo wenye lengo la
    kuongeza kina cha gati utekelezaji wake umefikia asilimia 13. Kukamilika kwa mradi huo,
    kutaiwezesha bandari ya Tanga kuondokana na gharama kubwa za kuhudumia meli
    nangani.
    Bandari ya Mtwara
  8. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bandari ya Mtwara, awamu ya kwanza ya
    ujenzi wa gati moja lenye urefu wa mita 300 litakalohudumia shehena mchanganyiko
    umekamilika kwa asilimia 100. Aidha, ukarabati wa yadi ya kuhudumia shehena kupitia

11

ujenzi wa sakafu ngumu eneo la mita za mraba 5,600 na ukarabati wa ghala namba 3 nao
umekamilika.

  1. Mheshimiwa Spika, maboresho hayo yanayoendelea yana lengo la kuhakikisha
    Bandari ya Mtwara inakuwa endelevu kwa kusafirisha bidhaa na mazao yanayozalishwa
    mikoa ya Kusini ikiwemo zao kuu la korosho na mazao mengine kama ufuta na makaa ya
    mawe kutoka Ngaka. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imeongeza uwezo wa Bandari ya
    Mtwara kuhudumia shehena ambapo kwa sasa ina uwezo wa kuhudumia tani 1,000,000
    kwa mwaka ikilinganishwa na tani 400,000 za awali.
  2. Mheshimiwa Spika, upanuzi wa bandari ya Mtwara umeongeza uwezo wake na
    kuifanya iweze kuhudumia meli nne kwa wakati mmoja. Vilevile, maeneo ya wazi ya
    kuhudumia na kuhifadhi shehena yaliyosakafiwa yameongezwa hadi kufikia uwezo wa
    kuhudumia makasha 12,950 kwa wakati mmoja. Hali kadhalika, maghala ya kuhifadhi
    mizigo yaliyopo yana uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 kwa wakati mmoja.
  3. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zinazokwenda sambamba na maboresho hayo
    ni kupungua kwa tozo ya aridhia kwa mazao ya kilimo kutoka asilimia moja hadi asilimia
    0.5 ya mali pwani ikilinganishwa na bandari nyingine nchini. Vilevile, kuongeza muda wa
    makasha tupu kukaa bandarini kutoka siku 15 na kuwa muda wa kipindi chote cha msimu
    wa korosho na kuongeza muda wa makasha yenye mzigo kukaa bandarini bila tozo ya
    kuhifadhi kutoka siku saba hadi siku 15 na kupunguza ya tozo za kuhudumia meli na
    shehena kwa asilimia 30.
  4. Mheshimiwa Spika, maboresho yanayoendelea katika bandari ya Mtwara ikiwemo
    kuweka unafuu wa gharama za kuhudumia shehena yanalenga kuongeza matumizi ya
    bandari hiyo hususan katika usafirishaji wa mazao ya kilimo, jasi (gypsum), makaa ya
    mawe kutoka Ruvuma sambamba na kukuza shughuli za kiuchumi katika ushoroba wa
    Mtwara.
    Bandari za Maziwa Makuu
  5. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande mwingine imeendelea na uboreshaji wa
    bandari zilizopo kwenye maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ili ziweze kutoa
    huduma bora na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
  6. Mheshimiwa Spika, uboreshaji wa bandari mbalimbali katika Ziwa Victoria kupitia
    ujenzi wa gati, majengo ya utawala na abiria na maghala ya kuhifadhi mizigo katika
    bandari za Magarine (Muleba), Nyamirembe (Chato), Bukoba, Kemondo Bay, pamoja na
    ujenzi wa gati mbili katika bandari ya Mwigombero (Musoma) na gati moja katika bandari
    za Lushamba na Nkome umekamilika.
  7. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Ziwa Tanganyika, Mradi wa Uboreshaji wa
    Bandari ya Kibirizi na Ujiji umekamilika kwa asilimia 52 na ujenzi wa bandari ya Karema
    umekamilika kwa asilimia 55. Aidha, ujenzi wa miundombinu mingine ikiwemo majengo ya
    abiria na ghala la kuhifadhia mizigo katika bandari za Kasanga, Sibwesa, Kabwe, Kipiri na
    Lagosa (Mpanda Vijijini), Kabwe (Nkasi) na Ujiji unaendelea.
  8. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Ziwa Nyasa, ujenzi wa bandari na
    miundombinu mingine ikiwemo majengo ya abiria na ghala la kuhifadhia mizigo katika
    bandari ya Ndumbi umefikia asilimia 82.

12

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu na
    utoaji huduma za bandari ili kuongeza chachu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa letu.
    Hivyo basi, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi kwa ujumla
    kuendelea kumuunga Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano
    wa Tanzania na dhamira yake ya dhati ya kutuletea maendeleo.
    UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
  2. Mheshimiwa Spika, Taifa letu linaendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika
    fani za utamaduni, sanaa na michezo. Shughuli mbalimbali za utamaduni, sanaa na
    michezo zimeendelea kuling’arisha Taifa letu kwa viwango tofauti ndani na nje ya nchi.
  3. Mheshimiwa Spika, utamaduni wetu unatangazwa vyema kupitia shughuli
    mbalimbali za kijamii ikiwemo matamasha ya ngoma, mavazi, vyakula vya makabila
    mbalimbali n.k. Hivi karibuni Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo kiliendesha Tamasha la
    Utamaduni wa Mtanzania na lilipata mafanikio makubwa na mgeni rasmi alikuwa
    Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya
    Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia pia taasisi ya Tulia Foundation ya Mbeya, hivi
    karibuni iliandaa tamasha la ngoma za Utamaduni ambalo lilifana sana.
  4. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sanaa yapo maendeleo makubwa ikiwemo
    kuhusisha wasanii wengi ambao hujipatia kipato kupitia fani hiyo. Muziki wa aina zote,
    uchoraji, uchongaji na maendeleo ya filamu yamekuwa chachu ya kukua kwa sanaa yetu
    nchini. Hivi karibuni tulitembelewa na Msanii maarufu wa filamu Sanjay Dutt kutoka India
    kwa lengo la kuja kuanzisha ushirikiano na wasanii wa filamu wa Tanzania na India. Pia
    kutangaza utalii wetu. Bado yuko mbugani ambako anakagua maeneo ya kupiga picha na
    kutengeneza filamu ya mbunga zetu ili kulitangaza Taifa letu.
  5. Mheshimiwa Spika, kwenye michezo nako yako mafanikio makubwa yamefikiwa
    ambako michezo mbalimbali inaendelea kuchezwa. Timu za mpira wa miguu na mpira wa
    kikapu ziko kwenye Mashindano ya Kombe la Taifa chini ya udhamini wa CRDB kwenye
    michuano inayoendelea viwanja vya Chinangali hapa Dodoma, Timu za Taifa za Mpira wa
    Miguu kutoka mikoa mbalimbali zinaendelea na mashindano kwa ngazi mbalimbali. Kwa
    upande wa soka, timu zetu zimekuwa zikifanya vizuri. Ninawapongeza Twiga Stars kwa
    kufanikiwa kubeba kombe la COSAFA katika fainali zilizofanyika Afrika Kusini baada ya
    kuzifunga Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Botswana, Sudani, Zambia na Malawi, na kutoa
    mchezaji bora wa mashindano hayo ambaye ni Amina Bilali.
  6. Mheshimiwa Spika, timu yetu ya Wanawake ya Chini ya Miaka 20 “Under 20”,
    imefuzu hatua ya tatu ya kucheza Kombe la Dunia bado hatua mbili ambazo wakishinda
    watacheza Kombe la Dunia. Timu hii imeshika nafasi ya tatu katika mashindano ya
    CECAFA Under 20. Mchezaji wetu Aisha Masaka alipata tuzo ufungaji bora kwa kufunga
    magoli saba kwenye mchezo mmoja. Timu ya Vijana Under 20, walichukua ubingwa
    CECAFA Wanaume kwa kuifunga Congo goli moja.
  7. Mheshimiwa Spika, timu yetu ya Wanaume Taifa Stars inayoendelea na
    mashindano ya kufuzu hatua za awali za Kombe la Dunia imeondoka leo kwenda
    Madagascar kwa ndege maalumu na itacheza tarehe 14 Novemba, 2021. Licha ya
    kupoteza mchezo wao jana dhidi ya DR Congo, wameahidi kufanya vizuri dhidi ya
    Madagascar ili kuibakiza Tanzania kwenye viwango vya juu vya FIFA.

13

  1. Mheshimiwa Spika, vilevile, niungane na wapenda michezo na Watanzania wote
    kwa ujumla kuipa pongezi Taifa Stars kwa mafanikio makubwa waliyoyapata licha ya
    kupoteza mchezo wa jana dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
  2. Mheshiwa Spika, kuvunjika kwa koleo siyo mwisho wa uhunzi, hivyo nasi hatuna
    budi kuganga yajayo. Uongozi wa TFF, benchi la ufundi la Taifa Stars na wadau wote wa
    soka tutumie matokeo ya jana kujitathmini na kuja na mkakati bora wa kufanya vizuri zaidi
    katika mashindano yajayo. Tuendelee kuwekeza kwa vijana wetu, tuboreshe ligi yetu na
    tuimarishe vilabu vyetu ili tuweze kupata wachezaji bora ambao wanaweza kushindana na
    wenzetu katika medani za kimataifa.
  3. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwapongeza Watanzania kwa kufanya
    mabadiliko ya kitabia ya kupenda mazoezi ya viungo yanayofanywa kila pembe nchini kwa
    kushiriki marathon, jogging, mazoezi ya kutembea pia nyumba maalum za mazoezi (Gym).
    Napongeza sana wadhamini mbalimbali walioamua kudhamini timu za taifa, vilabu,
    makundi ya mazoezi, taasisi zilizoanzisha vikundi vya michezo, sanaa na utamaduni.
    Tunaanza kuona kuzuri tunakoelekea kuwa na Taifa la watu wenye afya timamu.
  4. Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu
    Hassan kwa kuwapongeza Twiga Stars na kuwapa viwanja vya kujenga nyumba wachezaji
    na waalimu wao hapa Dodoma. Nami niungane nawe Mheshimiwa Spika katika kuitakia
    heri timu yetu ya Bunge itakayoshiriki michuano ya Mabunge ya Afrika Mashariki huko
    Arusha, na hasa timu yetu ya wavutakamba.
    HITIMISHO
  5. Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kuwashukuru tena wote
    waliosaidia kufanikisha mkutano tunaoumaliza leo. Shukrani za pekee ni kwako wewe
    Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa
    kutuongoza vizuri katika kipindi chote cha mkutano huu wa tano.
  6. Mheshimiwa Spika, kipekee namshukuru Katibu wa Bunge, Bi. Nenelwa
    Mwihambi pamoja na watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha mkutano huu.
    Nawashukuru wale wote waliokuwa na jukumu la ulinzi na usalama ili kuhakikisha
    mkutano huu unafanyika na kumalizika salama. Napenda pia niwashukuru madereva wote
    kwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa. Ninawashukuru pia waandishi wa habari
    kwa kuhakikisha kuwa habari za hapa Bungeni zinawafikia wananchi kwa namna
    mbalimbali.
  7. Mheshimiwa Spika, mwisho, niwashukuru wananchi wa Dodoma na hasa wa Jiji
    la Dodoma kwa ukarimu wao wa kutupatia huduma zote muhimu na hivyo kutuwezesha
    kukamilisha mkutano huu kwa mafanikio makubwa. Nitumie nafasi hii sasa kuwatakia
    wote safari njema wakati mnarejea katika maeneo yenu ya kazi.
  8. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunaelekea mwishoni mwa mwaka na mkutano
    ujao wa Bunge utakuwa mwakani, naomba nitumie fursa hii kuwatakia Watanzania wote
    sikukuu njema ya Krismasi na heri ya Mwaka Mpya 2022. Tuendelee kumuomba Mwenyezi
    Mungu atuvushe sote na atufikishe salama mwaka 2022 ili tuweze kukutana tena katika
    Mkutano wa 6 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

14

  1. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako
    tukufu sasa liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 1 Februari, 2022 litakapokutana tena
    saa 3.00 asubuhi hapa jijini Dodoma.
  2. Mheshimiwa Spika,naomba kutoa hoja.
Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Latest Posts

Top Authors

Most Commented

Featured Videos

Translate »