HISTORIA UNDANI SAFARI YA MAISHA YA AUGUSTINO LYATONGA MREMA

HISTORIA UNDANI SAFARI YA MAISHA YA AUGUSTINO LYATONGA MREMA

Mwenyekiti wa chama cha TLP, Augustino Lyatonga Mrema (77) amefariki dunia leo Jumapili, Agost 21, 2022, saa 12.15 asubuhi. MWENDO ameumaliza! Augustino Lyatonga Mrema hatunaye tena! Amefikwa na mauti asubuhi ya Agosti 21, 2022 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mrema, mwanasiasa nguli wa siasa za Tanzania, amefikwa na umauti akiwa na

Mwenyekiti wa chama cha TLP, Augustino Lyatonga Mrema (77) amefariki dunia leo Jumapili, Agost 21, 2022, saa 12.15 asubuhi.

MWENDO ameumaliza! Augustino Lyatonga Mrema hatunaye tena! Amefikwa na mauti asubuhi ya Agosti 21, 2022 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mrema, mwanasiasa nguli wa siasa za Tanzania, amefikwa na umauti akiwa na umri wa miaka 77 na taarifa zinaeleza kwamba, alifikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Agosti 16, 2022 ambapo alikuwa akiendelea kupatiwa matibabu mpaka alipofikwa na mauti.

Ifuatayo ni historia ya Mrema, milima na mabonde aliyopitia mpaka alipofikwa na mauti.

Alipozaliwa Desemba 31, 1944 katika Kijiji cha Kiraracha, jirani kabisa na Mlima Kilimanjaro, wazazi wake walimpa jina la Augustino. Alizaliwa katika familia ya kawaida kabisa, akiwa mtoto wa pili kati ya watoto watano katika familia ya mzee Lyatonga Mrema.

Wakati anazaliwa, pengine hata wazazi wake hawakutarajia kwamba siku moja Augustino Lyatonga Mrema, anaweza kuja kuwa mtu mashuhuri katika siasa za Tanzania.

Alianza elimu ya msingi mwaka 1955 na kuhitimu darasa la saba mwaka 1963, Moshi mkoani Kilimanjaro. Baada ya hapo, alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Patrick, Moshi ambapo alihitimu mwaka 1965.

Baada ya hapo, aliajiriwa kuwa mwalimu na mwaka 1966 alijiingiza rasmi kwenye siasa. Akiwa anaendelea na kazi yake ya ualimu, alikuwa pia akiendelea na mafunzo ya elimu ya sekondari ambapo mwaka 1968, alifanya mtihani wa Kidato cha Nne kupitia programu ya Chuo Kikuu cha Cambridge.

Mwaka 1970, alijiunga na Chuo cha Siasa cha Kivukoni ambako aliendelea kunolewa katika masuala ya siasa na baada ya kuhitimu, aliendelea na kazi yake ya ualimu, akifundisha shule mbalimbali mkoani Kilimanjaro. Baadaye, alipandishwa cheo na kuwa mratibu wa elimu wa kata.

Baadaye, alichaguliwa kuwa mwalimu wa siasa, ambapo aliendelea na kazi hiyo huku akipanda ngazi, moja baada ya nyingine.

Mwaka 1980 hadi 1981, alienda nchini Bulgaria ambako alifanikiwa kutunukiwa Diploma ya Sayansi ya Ustawi wa Jamii na Utawala na aliporejea nchini, alijiunga na taasisi nyeti ya usalama wa taifa.

Akiwa usalama wa taifa, Mrema alitumikia nafasi mbalimbali, ikiwemo mwalimu wa siasa, afisa msaidizi wa usalama wa taifa katika Mkoa wa Dodoma ambapo baadaye alipandishwa cheo na kuwa afisa mkuu wa usalama wa mkoa wa Dodoma.

Baada ya hapo, alifanya kazi mbalimbali za kijamii na kichama kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Pacific mwaka 2003 ambako alitunukiwa Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Jamii.

Mwaka 1985, Mrema alirudi nyumbani kwao, Vunjo, Kilimanjaro na kugombea ubunge ambapo alipata ushindi mkubwa akawekewa pingamizi na mahakama kuu.

Wakati kesi ikiendelea, alipelekwa katika Mkoa wa Shinyanga, Wilaya ya Kahama ambako alitumika kama afisa wa serikali mpaka mwaka 1987 aliposhinda rufaa yake na kurejeshewa ubunge wake.

Aligombea ubunge kwa mara nyingine mwaka 1990 na akafanikiwa kutetea jimbo lake, tena safari hiyo kwa kishindo na akarudi bungeni kwa mara ya pili.

Baadae akateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia mwaka 1990, na wakati huohuo mwaka 1993 hadi 1994 aliteuliwa tena kuwa Naibu Waziri Mkuu, cheo ambacho hata hivyo hakikuwepo kwenye katiba ya nchi.

Ilipofika mwaka 1994 alibadilishwa wizara hiyo na kuhamishiwa katika Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo.

Mwaka 1995, Mrema alijiengua kutoka chama tawala cha CCM na kujiunga na Chama cha NCCR – Mageuzi ambako huko alienda kuwa Mwenyekiti wa Taifa na mgombea Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, akichuana vikali na Hayati Benjamin Mkapa ambaye alishinda.

Baadaye kulitokea mvurugano ndani ya NCCR Mageuzi, akaenda kuanzisha chama chake cha Tanzania Labour Part (TLP) ambako aligombea urais mara mbili, mwaka 2000 na 2005.

Mrema amewahi kuwa Mbunge wa Vunjo kwa vipindi kadhaa, mpaka mwaka 2015 alipoangushwa na James Mbatia.

Mwaka 2016, rais wa wakati huo, Hayati John Pombe Magufuli, alimteua Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Latest Posts

Top Authors

Most Commented

Featured Videos

Translate »