Serikali ya Zanzibar itaendeleza na kukuza sekta ya Michezo.

Serikali ya Zanzibar itaendeleza na kukuza sekta ya Michezo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza kwa vitendo azma yake ya kukuza na kuendeleza Sekta ya Michezo Nchini. Akikabidhi Tunzo kwa vilabu na wachwzaji walioibuka na ushindi katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar, Mhe. Hemed amesema Serikali kupitia Wizara ya

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza kwa vitendo azma yake ya kukuza na kuendeleza Sekta ya Michezo Nchini.

Akikabidhi Tunzo kwa vilabu na wachwzaji walioibuka na ushindi katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar, Mhe. Hemed amesema Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali ikiwemo kubuni na kuimarisha miundombinu ya michezo nchini ikiwemo ujenzi wa Viwanja vipya vya mpira wa miguu katika Wilaya zote za Zanzibar.

Amesema kwa kuwajali vijana na wapenzi wa michezo mbali mbali Nchini, Serikali kupitia wafadhali itajenga Viwanja vya Michezo sita kwa pamoja (six in one) vitakavyojengwa Unguja na Pemba hatua ambayo itatoa fursa kwa Vijana kuendeleza vipaji vyao katika Michezo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema umefika wakati kwa watendaji wa Shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar (ZFF)na Bodi ya ligi kubadilika kiutendaji ikiwemo kuviwezesha vilabu vyote ili viweze kucheza ligi iliyo bora sambamaba na kusimamia stahiki za makocha, waamuzi na wasimamizi wa ligi jambo ambalo litaepusha upangaji wa matokeo kabla ya ligi kuanza.

Amesisitiza Michezo ina umuhimu wa kipekee katika harakati zetu za kila siku, licha ya kutuburudisha lakini pia hujenga Afya hivyo Serikali itaendeleza Michezo ili kuifanya Zanzibar kuwa ni kituo cha mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuimarisha miundombinu na vituo vya taaluma za Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuweza kuimarisha Uchumi wake na kuzalisha ajira hasa kwa vijana.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali imeamua kuvifanyia ukarabati mkubwa Viwanja vya Amani Unguja na Gombani Pemba ili kuwa na ubora na vyenye viwango vinavyokubalika na Shirikisho la kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) hivyo ni wajibu wa ZFF kusimamia nidhamu hasa kwa mashabiki wanapokuwa uwanjani wakiangalia mpira ili kuepuka uharibifu wa miundombinu ambayo Serikali inatumia gharama nyingi kujenga na kuvifanyia ukarabati viwanja mbali mbali vya michezo.

Akitoa nasaha zake kwa wachezaji na Viongozi wa Michezo Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewanasihi wanamichezo kujiwekea mazingira bora ya kinidhamu na kujituma ili kujijengea sifa bora katika Soko la Michezo ndani na nje ya nchi na kuwataka kuendelea kujiepusha na vitendo viovu ili Taifa lipate wanamichezo bora wenye maadili na uzalendo katika kulitumikia Taifa lao.

Aidha Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kudhamini Ligi kuu ya Mpira wa Miguu Zanzibar kwa msimu wa Pili Mfululizo na kuitaka PBZ kuimarisha na kuendeleza udhamini huo ili kuongeza Ari na kukuza vipaji vya wanamichezo Nchini.

Mhe. Hemed amevipongeza vyombo vya Habari kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya ligi mbali mbali za ndani na je ya nchi ili wananchi waweze kupata Taarifa za michezo kwa muda muafaka.

Nae Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewatoa hofu wanamichezo kwa kusema Uwanja wa Amani unajengwa kwa viwango na ubora wa hali ya juu na Wizara itahakikisha Uwanja huo unatumika kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha Mhe. Tabia amesema Wizara inashirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kuhakikisha wanapata wadhamini ambao wataisaidia Serikali kunyanyua Michezo huku akiwaomba wadau wenginine wa michezo kudhamini ligi mbali mbali za Zanzibar.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar Ndg. Abdul-latif Ali Yassin amesema Shirikisho limepiga hatua kubwa sana kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa Michezo katika kutafuta fedha ambazo zinasaidia kuanzisha ligi mbali mbali na kwa ngazi tofauti.

Yassin amewataka Viongozi watakaochaguliwa kuliongoza Shirikisho hilo kuacha makundi yasiokuwa na tija na badala yake wahubiri umoja na mshikamano kwa vitendo jambo ambalo litasaidia kukuza soka la Zanzibar.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
04 July, 2023

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Latest Posts

Top Authors

Most Commented

Featured Videos

Translate »