HOTUBA YA WAZIRI MKUU MH, MAJALIWA LEO BUNGENI.

HOTUBA YA WAZIRI MKUU MH, MAJALIWA LEO BUNGENI.

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB.), WAZIRIMKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHAMKUTANO WA 13 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 10 NOVEMBA, 2023 JIJINI DODOMA UTANGULIZIShukurani Check Against Delivery 2 Check Against Delivery 3 Maswali na Majibu Tatu: Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB.), WAZIRI
MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA
MKUTANO WA 13 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TAREHE 10 NOVEMBA, 2023 JIJINI DODOMA

UTANGULIZI
Shukurani

  1. Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
    rehema kwa kutujalia uzima na afya njema na kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote za
    Mkutano wa 13 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama
    zilivyopangwa. Hivyo basi, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atupe hekima na nguvu
    ya kuweza kutekeleza maazimio yote yaliyopitishwa na Bunge lako tukufu.
  2. Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suhulu Hassan,
    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada za kutekeleza dhamira yake ya
    dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania. Sina shaka nyote mtakubaliana
    nami kuwa uongozi wake makini na busara zake zimeendelea kuchagiza maendeleo ya
    haraka ya uchumi wa nchi yetu pamoja na ustawi wa Mtanzania mmoja mmoja.
    Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya, ninawasihi
    Watanzania wote tuendelee kumuunga mkono ili aweze kutimiza dhamira yake.
  3. Mheshimiwa Spika, naomba pia nitumie fursa hii kumshukuru sana Dkt. Philip
    Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea
    kumsaidia Mheshimiwa Rais kutelekeza majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania.
    Ninampongeza sana Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa jitihada anazozifanya, ama kwa
    hakika busara zake zimekuwa chachu katika kuleta maendeleo ya haraka ya Taifa letu.
  4. Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie fursa hii kukupongeza sana kwa
    kuchaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani, IPU, katika kikao cha
    Baraza la Uongozi kilichofanyika tarehe   23 hadi 27 Oktoba huko Luanda, nchini Angola.
    Vilevile, ninakupongeza sana kwa kuwa Rais wa Tatu mwanamke kushika nafasi hiyo
    ambayo imeshawahi kushikwa na Mheshimiwa Najma Heptulla kutoka India (1999–2002)
    na Mheshimiwa Gabriela Cuevas kutoka Mexico (2017–2020). Kipekee ninakupongeza
    sana kwa kuwa Rais wa kwanza Mwanamke kutoka Afrika kuchaguliwa kushika nafasi hiyo
    kubwa ya Rais wa Mabunge Duniani.
  5. Mheshimiwa Spika, nirudie kukupongeza sana kwa ushindi huo ambao kwa
    hakika umetuletea heshima kubwa sana Watanzania kwani umeithibitishia Dunia nzima
    kuwa Watanzania tunao uwezo mkubwa wa uongozi na tunaaminika sana. Nitumie fursa
    hii kukutakia kila la heri Mheshimiwa Spika katika kutekeleza majukumu yako na niwasihi
    waheshimiwa wabunge wenzangu na Watanzania wote tuendelee kumwombea heri
    Mheshimiwa Spika.

Check Against Delivery

2

  1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukushukuru na kukupongeza sana
    kuendelea kuliongoza vema Bunge hili tukufu na kusimamia vema mijadala yote
    iliyoendeshwa katika Mkutano huu wa 13 tutakaouhitimisha hivi leo. Mwenye macho
    haambiwi tazama, hekima, ukomavu na weledi wako umeendelea kuongezeka siku hata
    siku. Hongera sana Mheshimiwa Spika!
  2. Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.),
    Naibu Spika kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukusaidia wewe Mheshimiwa Spika kutekeleza
    majukumu ya kuliongoza Bunge. Vilevile, niwashukuru Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge
    ambao ni Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb.) na Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb.).
  3. Mheshimiwa Spika, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu
    kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Bahati Ndingo, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kwa
    kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika hivi
    karibuni. Ushindi huo wa kishindo ni kielelezo tosha kuwa wananchi wa Jimbo la Mbarali
    bado wana imani kubwa kwa Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi. Vilevile,
    ninampongeza sana Mheshimiwa Aziza Sleyum Ally kwa kuteuliwa kuwa Mbunge wa Viti
    Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi. Nitumie fursa hii kukukaribisha sana, na kwa
    upande wetu, sisi Wabunge tunakuhakikishia kuwa tutakupa ushirikiano wa kutosha katika
    kutekeleza majukumu yako ya kuwatumikia wananchi.
  4. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitowashukuru
    Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kazi kubwa mliyoifanya. Mmeshiriki kikamilifu
    kutoka kamati, mijadala ambako hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa Mkutano huu.
    Michango yenu ni muhimu sana katika kuimarisha ustawi na huduma kwa Watanzania.
    Hivyo basi, niwahikishie kuwa Serikali imepokea michango yote, maoni pamoja na ushauri
    wenu ambao kimsingi umekuwa ukisaidia sana katika kutekeleza mipango na mikakati
    mbalimbali ya Serikali.
    Salamu za Pole
  5. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Septemba hadi Novemba 2023, wapo
    Watanzania wenzetu waliopatwa na majanga mbalimbali yakiwemo ajali za barabarani,
    moto na mengine yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali. Kwa masikitiko makubwa
    ninatoa salamu nyingi za pole kwa wahanga wote wa majanga hayo. Aidha, ninatoa pole
    kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao kutokana na masahibu hayo.
    Kwa wale majeruhi tuzidi kuwaombea uponyaji wa haraka na kwa marehemu tuwaombee
    kwa Mwenyezi Mungu ili azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina!
    SHUGHULI ZA BUNGE
  6. Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa 13 wa Bunge lako tukufu, ulipokea na
    kujadili taarifa mbalimbali kutoka kwa kamati za Kudumu za Bunge, maswali kutoka kwa
    Waheshimiwa Wabunge na majibu ya Serikali sambamba na kujadili na kupitisha miswada
    ya sheria.

Check Against Delivery

3

Maswali na Majibu

  1. Mheshimiwa Spika, kupitia mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliuliza
    maswali 154 ya msingi na mengine 454 ya nyongeza ambayo yalijibiwa na Serikali.
    Halikadhalika, maswali manne ya papo kwa papo yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na
    kujibiwa na Waziri Mkuu baada ya kuwa nimetoa taarifa kuhusu Kuidhinishwa kwa Sera ya
    Elimu na Mafunzo 2014, Tolea la 2023 na Mitaala ya Elimu ngazi ya Elimu ya Awali,
    Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu mbele ya Bunge lako tukufu.
    Miswada ya Sheria
  2. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako tukufu limepokea Miswada
    nane ya sheria kama ifuatavyo:
    Moja: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbakmbali (Na.4) wa Mwaka
    2023 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.4) Bill, 2023].
    Mbili: Muswada we Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Sekta ya Sheria
    wa Mwaka 2023 [The Legal Sector Laws (Miscellaneous Amendments) Bill,
    2023]

Tatu: Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote wa Mwaka 2023.
Nne: Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma wa Mwaka 2023.
Tano: Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka

2023.

Sita: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (5) wa Mwaka
2023(The Written Laws Miscellaneous Amendments) (No.5) Bill, 2023.
Saba: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka

2023 (The Political Affairs Laws (Ammendment) Bill, 2023.

Nane: Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023.
Maazimio ya Bunge

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 61 na 107 hadi 112 za Kanuni za
    Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023, na kwa kuzingatia wajibu wa Bunge katika
    kuisimamia na kuishauri Serikali, Bunge lako tukufu lilipokea, kujadili na kupitisha
    Maazimio mawili kama ifuatavyo:

Check Against Delivery

4

Moja: Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi
ya Dawa ya Afrika la Mwaka 2023 (Treaty for Establishment of the African
Medicines Agency – AMA).
Mbili: Azimio ta Bunge kuhusu Mapendekezo ya Tanzania Kundhia Kusunga na Mkataba
we Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu la Mwaka 2009 (Statute of the
Intemational Renewable Energy Agency – IRENA).

  1. Mheshimiwa Spika, Maazimio haya yalipokelewa na kujadiliwa na Waheshimiwa
    Wabunge kwa ustadi wa hali ya juu huku wakionesha nia njema ya kujenga mustakabali
    mwema wa taifa letu. Kwa dhati niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa kukubali
    kuridhia kupitisha maazimio haya.
    Taarifa za Serikali Bungeni
  2. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 56 ya Kanuni za Kudumu za Bunge
    Toleo la Februari 2023, Bunge lako tukufu katika Mkutano wa 13 lilipokea Taarifa ya
    Serikali kuhusu Kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Tolea la 2023 na
    Mitaala ya Elimu ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu niliyoitoa
    mbele ya Bunge lako Tukufu siku ya tarehe 3 Novemba 2023.
    Taarifa ya Kamati za PAC na LAAC kuhusu hesabu zilizokaguliwa na CAG kwa
    mwaka wa fedha 2021/2022 na Taarifa ya Kamati ya PIC kuhusu Uwekezaji
    na Mitaji ya Umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022
  3. Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa 13 wa Bunge lako ulipata nafasi pia ya
    kupokea na kujadili kwa kina Taarifa za Kamati za Bunge ikiwemo Kamati ya Kudumu ya
    Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za
    Mitaa (LAAC), na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kwa
    Mwaka wa Fedha 2021/2022 ulioishia tarehe 30 Juni, 2022. Taarifa hizi za Kamati
    zinazotokana na Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
  4. Mheshimiwa Spika, taarifa za Kamati hizi tatu zimechambua kwa kina hoja
    mbalimbali za ukaguzi zinazohusu matumizi ya fedha za umma kwa hesabu za Serikali
    Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma pamoja na mwenendo wa
    uwekezaji wa mitaji ya umma uliofanywa na taasisi za umma kwa mwaka wa fedha
    ulioiishia tarehe 30 Juni, 2022. Jumla ya maazimio 117 yaliyotokana na hoja 14
    yameweza kutolewa na Bunge, ambayo kimsingi ni maelekezo mahsusi kwa Serikali.
  5. Mheshimiwa Spika, niruhusu nitoe pongezi za dhati kwa ndugu Charles E.
    Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na Ofisi ya Taifa ya
    Ukaguzi kwa kuendelea kuwa taasisi yenye kuaminika inayotoa Huduma za Ukaguzi kwa
    kuzingatia viwango vya kimataifa. Nyote ni mashahidi kwamba, ofisi hii imendelea
    kujipambanua kwa namna inavyojenga, inavyokuza na kuimarisha utamaduni wa
    uwajibikaji katika kusimamia na kudhibiti ipasavyo ukusanyaji wa mapato na matumizi ya

Check Against Delivery

5

Serikali kama inavyoidhinishwa na Bunge katika Wizara na Taasisi za Serikali, Mikoa na
Halmashauri. Vilevile, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imeweza kuwahikikishia Watanzania na
jamii yote namna ambavyo nchi yetu inavyoweza kupata faida au tija kutokana na
matumizi bora ya fedha za Umma, na namna ambavyo mali za Umma zinahifadhiwa,
kutunzwa na kulindwa ipasavyo.

  1. Mheshimiwa Spika, niwashukuru Maafisa Masuuli pamoja na Watendaji wote
    wa Serikali kwa namna ambavyo wameweza siyo tu kujibu hoja za Ukaguzi ambazo
    zilibainishwa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, lakini pia
    kuweza kutekeleza takwa la Kikatiba la kufika mbele ya Kamati husika za Bunge kwa ajili
    ya ufafanuzi wa kina. Aidha, nitoe shukrani zangu kwa Waheshimiwa Mawaziri kwa
    michango yao katika kutoa majibu ya Serikali kwa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na
    Waheshimiwa Wabunge. Ni ukweli ulio bayana kwamba hoja zilizoibuliwa na
    Waheshimiwa Wabunge ni nyingi, muhimu na zote zinahitaji majibu na utekelezaji wa
    haraka. Niseme tu kuwa Serikali yenu ni sikivu na itatekeleza mapendekezo hayo kwa
    kutoa majibu sahihi na utekelezaji wa haraka.
  2. Mheshimiwa Spika, hivyo basi, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge pamoja
    na majibu yaliyotolewa na Serikali, mturuhusu tufanyie kazi masuala yote yanayohitaji
    mabadiliko ya kisera na kisheria. Na mabadiliko haya yote tutalishirikisha kikamilifu
    Bunge hili ili kutimiza ndoto na malengo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais
    wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu.
  3. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa
    Serikali baada ya kupokea hoja na maazimio yote, tayari imeandaa Bangokitita ambalo
    linaainisha jukumu la kila Wizara kwa ajili ya kufanyia kazi maelekezo ya Bunge ili
    kurahisisha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji kwa waheshimiwa wabunge rejea yao.
    Hivyo basi, ninaziagiza Wizara husika ziandae kwa wakati taarifa za utekelezaji wa
    Maazimio yote kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati. Ofisi ya Waziri Mkuu
    kwa upande wake, itaandaa taarifa ya Serikali ambayo itawasilishwa kwa Mheshimiwa
    Spika.
    Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha
    2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na
    Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
  4. Mheshimiwa Spika, pamoja na hoja za Kamati za Bunge zilizopokelewa na
    kujadiliwa na Waheshimiwa Wabunge, Serikali iliwasilisha Mpango wa Maendeleo wa
    Taifa na Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
    ambapo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuchangia hoja hii moja kwa moja na kwa
    maandishi. Ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao katika
    Mpango huu pamoja na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka
    2024/2025.

Check Against Delivery

6

  1. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Mipango ya Maendeleo ya kila mwaka
    ni nyenzo muhimu ya matumizi bora ya rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
    Mipango hii huhakikisha malengo ya Dira 2025 yanafuatiliwa na kusimamiwa kila mwaka
    ili kuweza kukuza uchumi na kuondoa umaskini nchini. Mapendekezo ya Mpango
    yameainisha maeneo mahsusi ya kipaumbele yatakayozingatiwa katika maandalizi ya
    Mpango na Bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa kuzingatia rasilimali zilizopo.
  2. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla katika mwaka 2024/2025 msisitizo utawekwa
    katika kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi; kuimarisha ushiriki wa Watanzania
    katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo. Vilevile, msisitizo utawekwa
    katika kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maandalizi na utekelezaji wa mipango,
    uwekezaji na uzalishaji nchini.
  3. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imewasilisha Mwongozo wa Maandalizi ya
    Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/2025. Mwongozo huu kimsingi ni maelekezo ya
    jumla na maelekezo mahsusi yanayopaswa kuzingatiwa na Maafisa Masuuli katika hatua
    zote za uandaaji, uwasilishaji, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini pamoja na utoaji wa
    taarifa za utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025.
  4. Mheshimiwa Spika, Mwongozo huu umejikita katika kuhakikisha Serikali
    inatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
    Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambavyo ni pamoja na: kuchochea uchumi shindani na
    shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza
    uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.
  5. Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango
    yao kwenye hoja hizi mbili ambazo kwa pamoja zinatoa mwelekeo wa wapi nchi yetu
    inataka kufika kwa kuangalia kule tulipotoka. Hivyo, nitoe rai kwa Maafisa Masuuli na
    watendaji wote wa Serikali kutafsiri kwa vitendo na kwa umakini mkubwa maelekezo
    yote yaliyotolewa na Bunge hili ikiwa ni sehemu ya kutimiza ndoto za Mheshimiwa Dkt.
    Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
    MASUALA YA UTABIRI WA HALI YA HEWA
  6. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa, mvua zimeanza kunyesha katika
    maeneo mbalimbali hapa nchini. Na tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeshatoa
    utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi
    Desemba 2023. Utabiri huo, umebainisha uwepo wa hali ya El Nino ambayo itaambatana
    na mvua kubwa na kusababisha mafuriko ambayo yanaweza kuleta athari mbalimbali
    zikiwemo; madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii, upotevu wa mali na uharibifu wa
    miundombinu.
  7. Mheshimiwa Spika, taarifa ya utabiri wa hali ya hewa inaonesha mvua hizo
    zitakuwa juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza,
    Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, kusini mwa Mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa

Check Against Delivery

7

Mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na kaskazini
mwa Mkoa wa Morogoro.

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kuzuia na
    kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na uwepo wa El Nino sambamba na
    kujiandaa kukabiliana na mvua hizo kubwa. Kwa msingi huo, nitumie fursa hii
    kuzielekeza Wizara, Mikoa na Taasisi za Serikali kuzingatia masuala yafuatayo:
    Moja: Kuainisha na kuandaa rasilimali za kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa

endapo yatatokea;

Mbili: Kuelimisha na kuhimiza wananchi kuhama kwenye maeneo hatarishi na

kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha na mali;

Tatu: Idara na Taasisi zinazohusika na mazingira na miundombinu zihakikishe
barabara zinapitika wakati wote, mitaro na makalvati yanaimarishwa na
kusafishwa ili kuruhu maji yapite;

Nne: Sekta za maji, umeme na mawasiliano ziweke mipango ya kuzuia madhara na

kuhakikisha uharibifu katika huduma hizo unapewa ufumbuzi mapema;

Tano: Kushirikisha wadau wa maafa ikiwemo wananchi, taasisi za umma na sekta

binafsi katika mipango yote ya usimamizi wa maafa;

Sita: Kutoa taarifa haraka kwa mamlaka husika inapotokea maafa katika sekta

husika;

Saba: Kamati za Maafa katika ngazi ya Kijiji, Wilaya, Mkoa na Taifa zijipange kikamilifu

kukabiliana na changamoto za El Nino endapo zitajitokeza;

Nane: Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri ziandae mipango ya utekelezaji
katika maeneo yao kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana
na Madhara ya El Nino.

  1. Mheshimiwa Spika, niwasihi wananchi wote kujenga utamaduni wa kufuatilia
    taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Viongozi na
    Mamlaka ya Hali ya Hewa ikiwemo kuhama kwenye maeneo hatarishi na kufanya
    shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama. Kwa upande mwingine, wananchi
    waendelee kuweka akiba ya chakula na kutumia mvua hizo nyingi kulima mazao
    yanayostawi katika mazingira ya maji mengi.
    HALI YA UKUSANYAJI WA MAPATO
  2. Mheshimiwa Spika, uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kutokana na
    hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo kuwezesha

Check Against Delivery

8

uwekezaji wa kimkakati katika sekta za uzalishaji, huduma za jamii na miundombinu.
Ukuaji huo wa uchumi umechangia kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta rasmi na isiyo
rasmi na hivyo, kuiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi.

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024,
    mapato kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje yalifikia shilingi trilioni 9.06, sawa na
    asilimia 89.6 ya lengo la kipindi hicho. Kati ya kiasi hicho, mapato ya ndani yalikuwa
    shilingi trilioni 6.94 sawa na asilimia 96.2 ya lengo la kipindi hicho. Mapato ya ndani
    yanajumuisha shilingi trilioni 6.15 zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania;
    shilingi bilioni 491 za mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Wizara, Idara
    zinazojitegemea na Taasisi; na shilingi bilioni 299 kutoka vyanzo vya Mamlaka za Serikali
    za Mitaa.
  2. Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa mapato kunatokana na juhudi kubwa
    zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo kuimarisha mifumo ya ukusanyaji
    wa mapato na kurahisisha ulipaji wa kodi. Katika hatua nyingine, kuimarika kwa mapato
    kumewezesha Serikali kuendelea kuwahudumia wananchi kupitia ujenzi na uboreshaji wa
    miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.
  3. Mheshimiwa Spika, vilevile, mapato hayo yamewezesha ujenzi wa reli ya kati
    kwa kiwango cha kimataifa; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere;
    uboreshaji wa miundombinu ya barabara na reli; mpango wa Elimumsingi na Sekondari
    bila ada; kuboresha Shirika la Ndege la Tanzania; usambazaji umeme vijijini na mikopo
    ya wanafunzi wa elimu ya juu.
  4. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili
    kuhakikisha kuwa malengo ya makusanyo na utekelezaji wa bajeti kwa ujumla
    yanafikiwa. Mikakati hiyo ni pamoja na: kuimarisha mifumo ya usimamizi na ukusanyaji
    wa mapato; kuimarisha doria maeneo ya mipakani; kutoa elimu kwa walipa kodi kuhusu
    umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari; kuhimiza matumizi ya stakabadhi za kielektroniki za
    EFD na kuendelea kuboresha mazingira ya kuvutia uwekezaji na biashara.
  5. Mheshimiwa Spika, vilevile, mikakati hiyo inalenga kuhakikisha taasisi zenye
    sura za utoaji wa huduma kwa pamoja zinaboresha mifumo ya ukusanyaji kwa
    kuwezesha kutoa namba ya malipo jumuishi ili kurahisisha ulipaji kodi, ada na tozo
    mbalimbali kwa wateja na hivyo kuongeza uhiari wa ulipaji kodi; na kuendelea
    kusimamia na kutekeleza kikamilifu sera za bajeti na fedha.
  6. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa
    kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuimarisha mifumo ya
    udhibiti wa ndani ili kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato. Aidha, Mamlaka hizo
    ziimarishe ushirikiano na Taasisi nyingine za umma kwenye ukusanyaji wa mapato
    ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Check Against Delivery

9

  1. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee niwashukuru wananchi kwa
    kushirikiana na Serikali katika ukusanyaji wa mapato ambayo ndiyo msingi wa
    maendeleo yetu. Vilevile, niwapongeze kwa dhati watumishi wa taasisi zenye dhamana
    na ukusanyaji wa mapato zikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka za
    Serikali za Mitaa kwa kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Aidha, niwasihi
    watumishi wote waliopewa dhamana hiyo kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu na
    kuendelea kutoa elimu ya mlipakodi ili kufanikisha ulipaji wa kodi kwa hiyari
    USIMAMIZI WA ELIMUMSINGI
  2. Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kuwa mojawapo ya malengo ya elimu
    nchini Tanzania ni kutoa elimu bora itakayowajengea uwezo wahitimu kushiriki kikamilifu
    katika shughuli za kiuchumi. Hatua hiyo itawezesha Taifa letu kufikia uchumi wa viwanda
    ifikapo mwaka 2025.
  3. Mheshimiwa Spika, Serikali katika kutekeleza azma hiyo, imekuwa ikifanya
    jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu; kutekeleza
    mpango wa elimumsingi na kidato cha tano na sita bila ada; kuongeza ajira za walimu
    na wakufunzi wenye sifa; kutoa ufadhili na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na
    maboresho ya sera na mitaala.
  4. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia uandikishaji wa wanafunzi
    kuanzia ngazi ya elimu ya awali bila kusahau watoto wenye mahitaji maalum ambapo
    zoezi ambalo huanza mwezi Oktoba kila mwaka. Kwa mwaka 2024, Serikali inatarajia
    kuandikisha Watoto wa Elimu ya Awali 1,877,484 wenye rika lengwa wakiwemo
    wavulana 934,560 na wasichana 942,924 na Darasa la Kwanza 1,729,180 wakiwemo
    wavulana 860,870 na wasichana 868,310.
  5. Mheshimiwa Spika, hadi sasa jumla ya watoto wa elimu ya awali 407,138 sawa
    na asilimia 21.7 wakiwemo wavulana 201,244 na wasichana 206,253 wameandikishwa.
    Kati ya watoto wa elimu ya awali walioandikishwa watoto wenye mahitaji maalum ni 960
    kati yao wavulana ni 488 na wasichana ni 472.
  6. Mheshimiwa Spika, watoto wanaotarajia kujiunga darasa la kwanza
    walioandikishwa ni 593,452 sawa na asilimia 34.3 wakiwemo wavulana 293,728 na
    wasichana 299,724. Kati ya wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa wenye
    mahitaji maalum ni 1,365 wakiwemo wavulana ni 733 na wasichana 632.
  7. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa yote nchini
    kusimamia zoezi la uandikishaji katika maeneo yao ambalo itakuwa vema likihitimishwa
    tarehe 31 Desemba 2023. Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha wazazi/walezi wote
    wenye Watoto wenye rika lengwa kuwaandikisha Watoto hao ili waweze kuanza masomo
    ifikapo Januari, 2024.

Check Against Delivery

10

  1. Mheshimiwa Spika, ninatoa wito kwa wadau wote wa maendeleo zikiwemo
    Taasisi za Kidini na Taasisi za Kiraia kushiriki katika kutoa hamasa kwa Watanzania nchi
    nzima ili watoto wote wenye rika lengwa waweze kuanza masomo mwezi Januari.
  2. Mheshimiwa Spika, jitihada hizo zinaenda sambamba na kukamilisha
    maandalizi yote muhimu ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2024
    ikiwemo ujenzi wa miundombinu. Jumla ya wanafunzi 1,206,995 sawa na asilimia 86.4
    ya wanafunzi 1,397,370 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi
    mwaka 2023 wanatarajiwa kujiunga na Elimu ya Sekondari Januari, 2024.
  3. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha Waheshimiwa Wakuu wa
    Mikoa wote nchini wahakikishe kuwa ujenzi wa miundombinu yote katika Shule za
    Sekondari unakamilika kabla ya tarehe 30 Novemba 2023. Serikali itachukua hatua kali
    kwa wote watakaoshindwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika Shule za
    Sekondari. Wakuu wa Mikoa fanyeni ufuatiliaji, Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya
    ujenzi katika Halmashauri zote nchini hivyo hakuna sababu wala visingizio vya
    kutokamilisha ujenzi kwa wakati.
    MIKOPO YA ELIMU YA JUU
  4. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu
    ya kati na ya juu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata mikopo ya wanafunzi.
    Katika mwaka wa masomo 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 786 kwa ajili ya
    mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati.
  5. Mheshimiwa Spika, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 731.3 zitatolewa kama
    mikopo kwa wanafunzi 220,376 wa shahada mbalimbali; shilingi bilioni 6.7 kwa
    wanafunzi 1,200 wanaofadhiliwa kwa mpango wa Samia Scholarship; na shilingi bilioni
    48 kwa wanafunzi wa stashahada zenye uhitaji mkubwa wa rasilimaliwatu nchini.
  6. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo
    kwa wanafunzi ambapo katika mwaka wa masomo 2023/2024 utoaji wa mikopo
    umehusisha wanafunzi wa stashahada. Dirisha la kupokea maombi ya mkopo kwa
    wanafunzi wa stashahada lilifunguliwa tarehe 7 Oktoba 2023 na kufungwa tarehe 29
    Oktoba 2023. Hadi dirisha linafungwa jumla ya waombaji 12,910 walikuwa
    wamewasilisha maombi.
  7. Mheshimiwa Spika, kwa upande shahada hadi tarehe 5 Novemba 2023 jumla
    ya wanafunzi 169,180 sawa na asilimia 77 ya lengo walikuwa wamepangiwa mikopo
    yenye thamani ya shilingi bilioni 555.8. Kati yao, wanafunzi 73,078 ni wapya wa shahada
    za kwanza na wengine 96,102 ni wanufaika wanaoendelea na masomo ambao matokeo
    yao ya ufaulu wa mitihani na kuendelea na masomo yamepokelewa na Bodi ya Mikopo.
  8. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi ya
    Teknolojia kusimamia kikamilifu zoezi la utoaji wa mikopo na kuhakikisha kuwa zoezi hilo

Check Against Delivery

11

linakamilika kwa wakati sambamba na kushughulikia kwa wakati changamoto za utoaji
wa mikopo kwa wanafunzi pale zinapojitokeza.

  1. Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi kuwawezesha vijana
    wa Kitanzania kupata elimu ya juu, bado kuna baadhi ya waajiri na wanufaika wa
    mikopo ambao hawatimizi wajibu wao wa kurejesha fedha waliokopeshwa ili mfuko
    uweze kusomesha vijana wengi zaidi. Hivyo basi, nitoe wito kwa waajiri na wanufaika
    wadaiwa wote kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kurejesha mikopo hiyo kwa hiyari.
    KUIMARISHA MAZINGIRA YA BIASHARA
  2. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili
    kuimarisha na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Sote tumeshuhudia
    mabadiliko ndani ya Serikali yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais, kwa kuanzisha Ofisi ya
    Rais, Mipango na Uwekezaji ili kuimarisha uratibu na kuongeza imani zaidi kwa
    wawekezaji.
  3. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuimarisha uwekezaji nchini ninaomba nitumie
    fursa hii kusisitiza masuala yafuatayo:
    Moja: Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kupitia Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC)
    kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, NIDA,
    BRELA, TRA, Idara ya Kazi, Idara ya Uhamiaji, NEMC, TANESCO, TBS, OSHA na
    TMDA, iboreshe mwongozo wa uwekezaji ili kubainisha fursa kulingana na
    mazingira ya sasa na kuzingatia taratibu za kuwatambua na kuwasajili
    wanaotaka kuwekeza nchini;

Mbili: Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) kiimarishe matumizi ya TEHAMA ili
kutangaza fursa nyingi za uwekezaji zilizopo nchini na kuwawezesha wawekezaji
kutumia TIC kama kiungo cha kupata taarifa muhimu kutoka kwenye taasisi za
Serikali nchini; na

Tatu: TIC ihakikishe kuwa mwongozo wa uwekezaji unapatikana kwa urahisi kwa

wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
MASUALA YA MAENDELEO YA VIJANA

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuratibu shughuli za Maendeleo ya
    vijana sambamba na kuandaa mfumo wa kitaifa wa uratibu wa afua zinazotekelezwa na
    Wadau mbalimbali. Mfumo huo utasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati na
    kuwawezesha vijana kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi.
  2. Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi imetoa
    mafunzo kwa vijana 121,898. Katika kipindi cha 2017 hadi 2023 vijana 91,106 wamepata
    ujuzi kwa njia ya uanagenzi. Vilevile, vijana 22,296 wamerasimishiwa ujuzi uliopatikana

Check Against Delivery

12

katika mfumo usio rasmi. Licha ya hayo, vijana 6,300 wamepata mafunzo ya uzoefu
kazini na vijana 2,196 waliokuwa kazini wameongezewa ujuzi. Pia, kupitia Mpango wa
Jenga Kesho iliyobora vijana 812 wamedahiliwa na wanashiriki mafunzo ya Kilimo
Biashara.

  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Mfuko
    wa Maendeleo ya Vijana imetoa mikopo ya shilingi bilioni 1.88 kwa miradi 85 yenye
    vijana 595. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imeendelea kutoa mikopo
    ambapo hadi kufikia Oktoba 2023 shilingi bilioni 1.27 zimetolewa kwa miradi 56 yenye
    vijana 392.
    BARAZA LA TAIFA LA BIASHARA
  2. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Sekta Binafsi, Serikali
    imeendelea kuweka mazingira wezeshi na kutengeneza fursa ya majadiliano kati ya Sekta
    Binafsi na Sekta ya Umma kupitia Baraza la Taifa la Biashara. Baraza hilo huandaa vikao
    vya majadiliano rasmi kufikia muafaka kati ya sekta hizo kuhusu maboresho ya mazingira
    ya biashara, uwekezaji na uchumi kwa ujumla.
  3. Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada hizo baraza limeongeza ushiriki wa
    Sekta Binafsi kupitia mfumo rasmi na jumuishi wa majadiliano katika ngazi zote za
    utawala. Vilevile, Baraza limewezesha Mikoa 11 kuratibu na kufanya mikutano ya
    Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya.
  4. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa maazimio ya Baraza umewezesha kufanya
    mapitio sera, sheria, kanuni, taratibu na mifumo mbalimbali; kuunganisha majukumu ya
    taasisi yanayoingiliana; kuimarisha vituo vya huduma za mahali pamoja; kuanzisha na
    kuunganisha mifumo ya TEHAMA na kuimarisha na kuongeza ushiriki wa Watanzania
    kwenye shughuli za kiuchumi hususan miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali.
    MKAKATI WA KUENDELEZA WANANCHI KIUCHUMI
  5. Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zilizochukuliwa na Serikali katika kutoa
    mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ikiwa ni sehemu ya uwezeshaji kwa wananchi
    wetu, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwaendeleza wananchi
    kiuchumi.
  6. Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)
    ambalo limeanzishwa chini ya Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Na. 16
    ya mwaka 2004. Sambamba na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji
    Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004, limepewa dhamana ya kuratibu, kufuatilia na
    kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi ambazo ni
    mtambuka na zenye kuhusisha wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi.

Check Against Delivery

13

  1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Septemba, 2023, mifuko na programu za
    uwezeshaji ilifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 743.7 kwa
    wanufaika wapatao 6,064,957 ambapo wanawake ni asilimia 54. Aidha, kwa mwaka
    2022/2023, mifuko na programu za uwezeshaji ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi
    bilioni 743.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 713.8 zilizotolewa mwaka 2021/2022. Hii ni
    sawa na ongezeko la asilimia 4.02.
    UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA
  2. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha na kuchochea shughuli za maendeleo
    nchini, Serikali imeendelea kuimarisha uhusiano wa kikanda na kimataifa kwa lengo
    kufungua fursa mbalimbali ikiwemo uwekezaji na mitaji katika sekta za utalii na
    uchukuzi. Katika hili, nimpongeze kwa dhati Mwanadiplomasia namba moja, Mheshimiwa
    Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari
    wa mbele kuimarisha diplomasia ya uchumi.
  3. Mheshimiwa Spika, masuala yanayozingatiwa kwenye diplomasia ya uchumi ni
    pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa zetu, kutafuta fursa za kiuchumi katika sekta
    mbalimbali, fursa za elimu, mafunzo, utaalamu na ujuzi pamoja na ajira nje ya nchi na
    kubidhaisha lugha ya Kiswahili.
  4. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2022/2023, Serikali iliratibu na
    kufanikisha kusainiwa kwa mikataba 13 na Hati za Makubaliano 37. Mikataba na hati hizo
    zinagusa sekta za kiuchumi na kijamii ikiwemo ulinzi na usalama, kilimo na uvuvi,
    viwanda, biashara, uwekezaji, TEHAMA na utalii. Nyingine ni afya, elimu, uchukuzi,
    mawasiliano, utamaduni, sanaa na michezo, sayansi na teknolojia, mazingira na uchumi
    wa buluu.
  5. Mheshimiwa Spika, ziara zinazofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu
    Hassan na viongozi wengine zimekuwa chachu ya kuimarisha uhusiano wa kimataifa.
    Vilevile, ziara hizo zimeibua fursa zenye manufaa ya kiuchumi nchini. Baadhi ya
    mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni ongezeko la watalii, ongezeko la wafanyabishara
    na wawekezaji, miradi mikubwa na ya kati, uwekezaji na kufungua masoko ya bidhaa
    mbalimbali. Kipekee, nimpongeze tena Mheshimiwa Rais wetu ambaye kupitia ziara zake
    na nchi jirani, aliweza kutatua changamoto za kibiashara kwenye mipaka ya Kenya na
    Zambia.
  6. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu na kufanikisha ziara za kikazi
    na kitaifa za Viongozi Wakuu kutoka mataifa mengine kuja hapa nchini. Baadhi ya
    viongozi hao walitoka Ujerumani, Indonesia, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
    Congo, Rwanda, Afrika Kusini, Falme za Kiarabu, Uswisi na Marekani.
  7. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuratibu ziara za Viongozi Wakuu wa
    nchi nyingine wanaozuru Tanzania ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya

Check Against Delivery

14

Tanzania na nchi nyingine. Ziara hizo zitaimarishwa ili nchi yetu iendelee kunufaika na
fursa za kiuchumi na kijamii lakini pia iweze kung’ara kikanda na kimataifa.
MAELEKEZO MAHSUSI

  1. Mheshimiwa Spika, wakati nikielekea kuhitimisha hotuba yangu naomba sasa
    niweke msisitizo katika masuala muhimu yafuatayo ambayo ni uratibu wa upatikanaji wa
    pembejeo; udhibiti na utatuzi wa migogoro ya ardhi; uhifadhi wa mazingira na
    kuimarisha mazingira ya biashara.
    Kuimarisha Uratibu wa Upatikanaji wa Pembejeo
  2. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa pembejeo
    muhimu kwa wakulima zikiwemo mbolea. Hadi kufikia tarehe 31 Oktoba, 2023, wakulima
    zaidi ya milioni 3.6 walikuwa wamesajiliwa na kupata namba za utambulisho za kununua
    mbolea ya ruzuku.
  3. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kupitia Bunge lako tukufu kuwaelekeza
    Wakuu wa Wilaya ambao pia ni Wenyeviti wa Kamati za Pembejeo za Wilaya
    wawahamasishe wakulima kujisajili na kutoa taarifa sahihi kuhusu mazao wanayolima na
    ukubwa wa mashamba yao kwenye madaftari ya wakulima ambayo yamesambazwa kwa
    watendaji wa vijiji na mitaa ili taarifa zao ziweze kuingizwa kwenye mfumo na wapatiwe
    namba za kununulia mbolea ya ruzuku.
  4. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuielekeza Wizara ya Kilimo ihakikishe
    mbolea inapatikana kwa wakati na ishirikiane na Wakuu wa Wilaya kusimamia kwa
    karibu usambazaji wa mbolea kwa wakulima. Hatua hii iende sambamba na kutatua
    changamoto zinazojitokeza wakati wa usambazaji wa pembejeo hiyo muhimu.
  5. Mheshimiwa Spika, vilevile, kampuni na taasisi zinazozalisha mbegu bora
    ziongeze kiwango cha uzalishaji na kuweka utaratibu mahsusi wa kufikisha mbegu hizo
    kwa wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji.
    Udhibiti na Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi
  6. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya
    kushughulikia migogoro ya ardhi kwa kushirikisha Wizara za kisekta. Mikakati hiyo ni
    pamoja na kuunda kamati maalum za kushughulikia migogoro, kuendesha kliniki maalum
    za ardhi ambapo wananchi wamekuwa wakisikilizwa malalamiko yao na kupatiwa
    ufumbuzi.
  7. Mheshimiwa Spika, mikakati mingine inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na
    kufanya vikao na wadau mbalimbali kuhusu usimamizi bora wa ardhi; kufanya kaguzi za
    milki; kutoa elimu kwa umma kuhusu utatuzi wa migogoro kwa kushirikiana na viongozi

Check Against Delivery

15

wa Serikali za Mitaa na kuwajengea uwezo watumishi ili kuimarisha huduma zitolewazo
kwa jamii.

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwachukulia hatua watumishi
    wanaochochea migogoro kwa kutozingatia sheria na kanuni na taratibu ikiwemo
    kujihusisha na vitendo vya rushwa. Vitendo hivyo havikubaliki kwani ni kinyume na
    maadili ya utendaji wa watumishi wa umma. Hivyo basi, nitumie fursa hii kumwagiza
    Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuwachukulia hatua kali watumishi
    wa idara za ardhi wanaokiuka sheria. Hivyo basi, kila mmoja akafanye kazi kwa weledi,
    uadilifu na kwa kuzingatia taaluma yake.
  2. Mheshimiwa Spika, nilitoa maelekezo kwamba kampuni zote zilizopewa kazi za
    upimaji wa viwanja kwenye Majiji, Manispaa na Mikoa na zimeshindwa kukamilisha kazi
    hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba ama hazikuwa na mikataba zichukuliwe hatua kali za
    kisheria. Ikumbukwe kuwa, kampuni nyingi zilizopewa kazi za kupima maeneo ya
    wananchi kwa lengo la kutoa hati miliki kote nchini hazifanyi kazi hizo kikamilifu licha ya
    wananchi kulipa fedha kwa muda mrefu, nasisitiza kuwa kampuni hizo zikuchukuliwe
    hatua za kisheria ikiwemo kuziachisha hizo.
  3. Mheshimiwa Spika, nilielekeza pia kwamba, Halmashauri zote kama mamlaka
    za upangaji ziongeze udhibiti na usimamizi wa maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya
    matumizi ya umma na yale ya hifadhi ya mazingira, yakiwepo maeneo ya ukanda wa
    kijani, maeneo ya wazi, viwanja vya michezo, makaburi na mengineyo ili kuzuia uvamizi
    na mabadiliko ya matumizi ya maeneo hayo. Mfano halisi ni Jiji la Dodoma na Manispaa
    ya Kigoma.
    Maeneo yote yaliyotengwa na kuhifadhiwa yasiruhusiwe kufanyiwa mabadiliko ni vema
    mabadiliko hayo yawe yamerishiwa na Kamati za Usalama za Mikoa na Wilaya kabla ya
    kuwasilishwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
    MICHEZO
  4. Mheshimiwa Spika, kipekee nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa
    Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono
    mapana aliyonayo katika kuinua Sekta ya Michezo hapa nchini. Mheshimiwa Rais, katika
    vipindi mbalimbali amekuwa akitoa miongozo ambayo imekuwa na tija na hatimaye
    kuleta mapinduzi makubwa katika ya sekta ya michezo. Sina shaka mtakubaliana nami
    kuwa kupitia maono yake, tasnia ya Michezo nchini inaendelea kuthaminiwa na
    tumeendelea kushuhudia matunda mazuri kwa timu zetu zikiwemo zile za Taifa.
  5. Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa ili timu zetu za taifa ziweze kushiriki
    katika michuano ya kimataifa, maandalizi ya kutosha yanahitajika ambayo yanagharimu
    fedha nyingi. Ninatoa pongezi kubwa sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
    Jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano

Check Against Delivery

16

wa Tanzania kwa kufanya maamuzi sahihi ya kuiwezesha timu ya Taifa ya Tanzania
kufuzu katika Fainali za AFCON.

  1. Mheshimiwa Spika, aidha, Mheshimiwa Rais amekuwa akiridhia ujumbe
    maalumu wa Serikali kuambatana na Taifa Stars katika michezo yao ya ugenini ili
    kuongeza hamasa kwa wachezaji na matokeo kweli tumeyaona. Ninampongeza sana
    Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutoa motisha kwa wanamichezo wetu ambazo
    zimekuwa zikiongeza ari na hamasa kwa wanamichezo wetu. Licha ya kuendeleza
    mpango wa Goli la Mama, mtakumbuka Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo
    tarehe 4 Oktoba 2023 alinituma nikatekeleze ahadi yake ya kuwatunuku Timu ya Taifa
    Stars fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwa kufuzu kushiriki mashindano ya Mataifa ya
    Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Ivory Coast Januari, 2024.
  2. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, mafanikio katika sekta ya michezo
    hapa nchini yamechagizwa pia michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo imekuwa
    ikitolewa ili kuboresha sekta ya michezo nchini. Sote tu mashuhuda jamii sasa
    imehamasika na ushiriki katika michezo na umeongezeka. Michezo imekuwa zaidi ya
    burudani kwani sasa ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi kusaidia kutatua changamoto
    mbalimbali katika Jamii ikiwemo ile ya ajira kwa vijana.
  3. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Baraza
    la Michezo la Taifa (BMT) katika kutekeleza mikakati ya maendeleo ya michezo hapa
    nchini Tanzania. Ushirikiano unaotolewa kwa taasisi za michezo umekuwa chachu ya
    kufanikiwa kutimiza malengo yetu ya kuendeleza michezo.
    Mfano mzuri ni ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya Michezo kwa sekata ya umma na
    binafsi. Kwa mfano Azam Complex, taasisi za ulinzi, taasisi za elimu kwa mfano shule,
    vyuo na taasisi nyinginezo.
  4. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kutoa pongezi nyingi kwa TFF kwa
    uzinduzi wa Mashindano ya Ligi ya Soka ya Afrika uliofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe
    20 Oktoba katika Uwanja wa Benjamin William Mkapa ambao haujawahi kutokea. Katika
    mechi hiyo ya uzinduzi Klabu ya Simba ilichuana na klabu ya Al Ahly ya Misri na kutoka
    sare.
  5. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuipongeza sana Timu ya Taifa ya soka
    ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20 almaarufu Tanzanite Queens kwa ushindi wa
    mabao 7 kwa 0 dhidi ya Djibouti katika mchezo wa kufuzu kombe la Dunia uliochezwa
    Uwanja wa Azam Complex tarehe 11 Oktoba, 2023. Kwa ushindi huo, Tanzanite Queens
    watachuana na Nigeria katika pambano litakalofanyika nchini Colombia mwaka 2024.
  6. Mheshimiwa Spika, ninawapongeza pia timu ya Twiga Stars kwa kusonga mbele
    katika hatua ya kufuzu mashindano ya WAFCON 2024. Ushindi huo umepatikana baada ya
    kupata ushindi wa penati 4 kwa 2 baada ya kuifunga timu ya Ivory Coast kwenye
    shindano lililofanyika pia katika Uwanja wa Azam Complex pale Chamazi Jijini Dar es

Check Against Delivery

17

Salaam. Aidha, ninawapongeza pia timu ya Twiga Stars kwa kufuzu mashindano ya
Olimpiki-2024 baada ya kuibwaga Botswana kwa bao moja bila katika mchezo uliofanyika
nchini Botswana.

  1. Mheshimiwa Spika, ninatoa pongezi nyingi kwa Timu ya wanawake ya JKT
    Queens kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Wanawake Ukanda wa Afrika Mashariki
    na Kati (CECAFA). Ubingwa huo umewawezesha kushiriki Ligi ya Mabingwa ya Wanawake
    Afrika inayoendelea nchini Ivory Coast.
  2. Mheshimiwa Spika, licha ya mchezo wa mpira wa miguu, ninawapongeza pia,
    vijana wetu Ramadhan Brothers wanasarakasi mahiri walioshiriki katika mashindano
    maarufu ya American Got Talent. Vijana wetu hawa wameonesha vipawa na uwezo wa
    hali ya juu katika mchezo huo na kukonga mioyo ya watazamaji wengi.
  3. Mheshimiwa Spika, washiriki wetu katika mchezo wa ngumi wameendelea
    kung’ara sana katika mashindano ya ndani na nje ya nchi yetu. Ninampongeza sana
    Mwanamasumbwi wetu Ibrahim Class kwa kushinda mkanda wa TPBRC baada ya
    kumshinda mpinzani wake Xiao Tau Su kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
  4. Mheshimiwa Spika, ninampongeza pia mwanasumbwi Pius Mpenda kwa
    kushinda ubingwa wa WBC Peace Champion baada ya kumshinda Mrusi Dauren
    Yeleussinov. Vilevile, ninampongeza sana Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ngumi
    Ngorongoro Black Rhinos Yusuf Lucas Changalawe kwa kufanikiwa kuingia katika fainali
    ya mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024.
  5. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mchezo wa mashindano ya mbio,
    ninampongeza sana mwanariadha wetu Magdalena Shauri kwa kushinda medali ya shaba
    katika mbio za BMW Berlin Marathon baada kushika nafasi ya tatu katika mbio hizo.
    Vilevile, ninampa pongezi nyingi Mwanariadha Alphonce Felix Simbu kwa kushika nafasi ya
    pili kwenye mashindano ya majeshi yanayojulikana kama The World CISM Half Marathon
    yaliyofanyika huko Uswisi. Ninawapongeza sana wanariadha wetu kwa ushindi huo
    mkubwa.
  6. Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro
    (Mb.) Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa
    kuendelea kusimamia vema utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais. Jitihada zenu
    zinaonekana kwani Tanzania inazidi kung’ara katika medani za kimataifa. Sote
    tunaendelea kushuhudia maendeleo makubwa ya sekta hii muhimu katika kuchangia Pato
    la Taifa na kukuza uchumi kwa ujumla.
    HITIMISHO
  7. Mheshimiwa Spika, ninapoelekea kuhitimisha hotuba yangu, nitumie fursa hii
    kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kufanya mjadala wa Bunge hili kwa
    kuzingatia manufaa makubwa ya ustawi wa taifa letu. Kama mnavyofahamu uwepo wa

Check Against Delivery

18

Bunge hili ulikuwa ni muhimu ili kuweza kupata maoni na ushauri kutokana na hoja za
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Aidha ninawashukuru watumishi wa Serikali kwa
kuendelea kufanyia kazi masuala mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwezesha uwasilishaji
wa hoja mbalimbali zilizotokana na mijadala ya Bunge hili.

  1. Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Katibu wa Bunge na Watumishi wote wa
    Bunge kwa huduma nzuri mliyotupatia katika kipindi chote cha Bunge hili. Kipekee,
    nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi yanu nzuri, kwa maana tumeishi kwa
    amani na utulivu katika kipindi chote cha Mkutano huu wa 13 wa Bunge la 12.
    Ninawashukuru sana wanahabari kwa kuendelea kuuhabarisha umma juu ya shughuli zote
    za Bunge letu Tukufu toka siku ya kwanza mpaka siku hii ya leo tunapoelekea kuhitimisha
    mkutano wetu. Pia natambua mchango mkubwa wa huduma unaotolewa na madereva
    wetu waliotuhudumia wakati wote. Pia ninatoa shukurani kwa watoa huduma wengine
    mlioshiriki kutuhudumia muda wote tukiwa hapa Dodoma.
  2. Mheshimiwa Spika, nirudie kukushukuru sana, wewe na Waheshimiwa Wabunge
    wenzangu, niwaahidi kuwa tutaendelea kutekeleza yale mliyoyashauri na kuyatolea maoni
    katika kipindi chote cha mkutano wa Bunge hili, kwani ushauri na maponi yenu ndio
    msingi wa kuiwezesha Serikali kutimiza majukumu yake ipasavyo. Nami niwatakie
    Waheshimiwa Wabunge wenzangu safari njema na mnaporejea majimboni kwenu na
    mkaendelee kuwahakikishia wananchi dhamira njema ya Rais wetu Dkt. Samia suluhu
    Hassan katika kuwaletea maendeleo Watanzania.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunaelekea mwishoni mwa mwaka, na hatutakuwa
    na Mkutano wa Bunge tena ndani ya mwaka 2023, nitumie fursa hii kuwatakia Watanzania
    na waumini wote wa Kikristo, sherehe njema ya sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wa
    2024.
  4. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa ninapenda kutoa hoja kuwa
    Bunge lako tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 30 Januari, 2024 saa tatu
    kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu hapa Jijini Dodoma.
  5. Mheshimiwa Spika sasa ninaomba kutoa hoja.
Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Latest Posts

Top Authors

Most Commented

Featured Videos

Translate »