MAJALIWA: VIONGOZI WA DINI WEKEZENI KATIKA MALEZI YA VIJANA.

MAJALIWA: VIONGOZI WA DINI WEKEZENI KATIKA MALEZI YA VIJANA.

9, Mei, 2021 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini katika mahubiri yao waweke msisitizo katika masuala ya kuwekeza kwa vijana ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo vyote hatarishi visivyozingatia maadili ya Mtanzania. “Tusisahau pia kwamba ukimwi bado upo. Aidha, vijana wengi wapo katika hatari ya kupata maambukizi. Kwa Msingi

9, Mei, 2021

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini katika mahubiri yao waweke msisitizo katika masuala ya kuwekeza kwa vijana ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo vyote hatarishi visivyozingatia maadili ya Mtanzania.

“Tusisahau pia kwamba ukimwi bado upo. Aidha, vijana wengi wapo katika hatari ya kupata maambukizi. Kwa Msingi huo, tumieni nafasi yenu katika jamii kutoa ushauri nasaha na hatimaye kupunguza kasi ya maambukizi kwa vijana”.

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 9, 2021) katika ibada ya kusimikwa kwa Askofu Dkt. Msafiri Mbilu, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Lushoto. Waziri Mkuu ameshiriki ibada hiyo kwa niaba ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi na majukumu makubwa ya Viongozi wa Kanisa ambayo ni pamoja na kuwaongoza watu kiroho na kuwapa mafundisho, ushauri na kuwajenga kiimani.

Mheshimiwa Majaliwa amesema “Hubirini masuala ya vijana kwani kauli yenu inapokelewa vizuri kwenye jamii na watu wa rika zote. Endeleeni kuwasaidia watu katika shida mbalimbali hususan wale wenye uhitaji kama yatima na wajane”.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi hao waendelee kutoa mafundisho yenye kuhimiza wananchi wadumishe amani na utulivu nchini kwa manufaa ya vizazi vya sasa na ya vizazi vijavyo.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inatambua kwamba maendeleo ya nchi hayawezi kwenda bila ya ushirikiano na sekta binafsi na kwa kuzingatia hayo, imekuwa ikishirikiana na Sekta binafsi zikiwemo Taasisi za dini katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa.

Amesema Serikali imekuwa ikishirikiana na Dayosisi hiyo katika utoaji wa huduma za afya kwenye hospitali zake zilizopo Bumbuli, Kilindi na Lutindi Mental Hospital kwa kutoa dawa pamoja na kuleta madaktari na watumishi ndani ya hospitali hizo ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma stahiki na kwa wakati.

“Nitumie nafasi hii tena kuwahakikishia kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano huu kwa manufaa ya Watanzania wote. Nitoe Rai kwa viongozi mnaowekwa wakfu leo kuwa viongozi wa Dayosisi hii ya Kaskazini Mashariki muendelea kuhubiri amani, upendo na mshikamano kwa wana Dayosisi na kwa Watanzania wote kwa ujumla”.

 Hizo ndizo Tunu alizotuachia Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambazo zilitunzwa na kuheshimiwa na viongozi wote waliopita, na zitaendelea kutunzwa katika awamu hii ya uongozi. Vilevile msichoke kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali kwa maendeleo ya jamii ya Watanzania”.

Kwa upande wake, Askofu Dkt. Mbilu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kushiriki katika ibada na amemuhakikishia kwamba Dayosisi yao itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo pamoja na kudumisha amani

(Mwisho)

IMETOLEWA NA

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, MEI 9, 2021.

Jfive Team
ADMINISTRATOR
PROFILE

Posts Carousel

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked with *

Latest Posts

Top Authors

Most Commented

Featured Videos

Translate »